NA SIMAI HAJI, MCC

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wilaya ya Kusini Unguja, AbdulAziz Ibrahim amewataka wanachama wa chama hicho kuwahamasisha wanachama wa vyama vua upinzani kukipigia kura chama hicho ili chama hicho kishinde kwa asilimia kubwa.

Alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wanachama na wapenzi wa CCM wa jimbo la Paje katika mwendelezo wa kampeni za uchaguzi mkuu utakaofanyika baadae mwezi huu.

“Tuendelea kuhamasishana lakini pia tuwahamasishe na wanachama wa vyama vya upinzani kuichagua CCM kwani ndicho chama chenye ilani inayotekelezeka,” alisema mwenyekiti huyo.

Akiomba kura katika mkutano huo, mgombea ubunge katika jimbo hilo,  Jaffar Sanya Jussa, aliwataka wanaCCM kuwa mstari wa mbele katika kulinda na kutunza amani iliyopo nchini jambo ambalo litaendelea kuipa haiba nzuri Zanzibar.

“Bila ya amani ni vigumu kutekeleza mipango ya maendeleo hicyo sisi tuwe vinara wa kuhubiri amani na usalama kwa maisha ya raia na mali zao,” alieleza.

Nae mgombea wa uwakilishi wa jimbo hilo, Dk. Sudi Nahoda aliwataka wananchi wa jimbo la paje kuwachagua wagombea wa CCM na kuwaahidi wananchi kuwa iwapo watawachagua viongozi wa katika jimbo hilo watakuza kilimo na kufikisha umeme katika maeneo ya mashamba.

“Endapo mtatuchagua tutajitahid kukikuza kilimo katika jimbo hili ikiwa ni pamoja na kusambaza umeme mashambani,” alisema mgombea huyo.