NA SAIDA ISSA, DODOMA

IKIWA Tanzania imeungana na mataifa mengine kuadhimisha siku ya Afya ya Macho Duniani, huku wito umetolewa kwa wananchi kuepuka kutumia dawa ya macho kiholela bila ya kuwa na maelekezo kutoka kwa Daktari.

Kauli hiyo ilitolewa kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali Profesa Abel Makubi, kwa vyombo vya habari katika kuadhimisha siku hiyo ,Mkurugenzi wa Idara ya Tiba Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Grace Maghembe, alisema ni muhimu mtu kufika hospitalini mara tu anapoona kuwa anamatatizo ya macho na sio kutumia dawa ambazo sio rasmi kwa ajili ya matibabu.

Alisema pamoja na kasi na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali, ili kuhakikisha wanafikisha huduma za macho katika maeneo mbali mbali hapa nchini tangu kuridhiwa kwa azimio hilo mnamo mwezi Mei 2003.

Wakati huo huo Dk. Maghembe, alisema inakadiriwa kuwa watanzania 600,000 hawaoni huku watu wenye matatizo ya kuona kwa kiwango cha kati na cha juu hapa nchini,, wanakadiriwa kuwa ni mara tatu ya watu wasioona ambao ni takriban milioni 1.8 hivyo kwa ujumla Tanzania ina watu milioni 2.4 wenye matatizo ya kuona na hapa.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa yasiyo ya kuambikiza Dk. James Kiologwe alisema, katika kuadhimisho siku hiyo wamejikita zaidi katika kutoa elimu, ili kusaidia watu kuchukua hatua za kujikinga kupoteza uoni wa macho.