NA TATU MAKAME
JESHI la Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kupatikana na dawa za kulevya.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Kamanda wa Polisi mkoa huo, Kamishna Msaidizi Haji Abdalla Haji, alisema tukio la kwanza lilitokea Septemba 29, mwaka huu majira ya saa 8:30 mchana.
Alisema katika tukio hilo Mbaraka Simba Khatibu (29) na Abdalla Mohamed Rashid (23) wakaazi wa Bumbwini Misufini wanashikiliwa na kwa tuhuma za kukamatwa na nyongo 16 za majani makavu yanayodhaniwa kuwa ni bangi yenye uzito wa gramu 8.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na kiwango hicho walihifadhi ndani ya mfuko wa buluu wenye maandishi ya MT “Turkey mfuko’ jambo ambalo ni kosa kisheria.
Katika tukio jengine Vuai Jaku Ame (40) mkaazi wa Chuini Wilaya ya MagharibI ‘B’ alipatikana na mirungi mafurushi 17 yakiwa kwenye gari yenye namba za usajili Z. 176 HR aina ya Super Custom.
Kamanda Haji, alieleza kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 25 mwaka huu, majira ya saa 9:40 usiku njia ya kuelekea Kendwa na kwamba mtuhumiwa huyo alikamatwa kufuatia operesheni iliyofanywa na kikosi cha kupambana na wauzaji na wasafirishaji wa dawa za kulevya.