NA ASYA HASSAN

WANAFUNZI wa kike kutoka skuli za zanzibar wameiomba serikali kuweka utaratibu utakaowawezesha kutoa maoni yao katika Baraza la Wawakilishi ili kupaza sauti zao.

Wakizungumza katika mkutano wa kujadili changamoto zinazowakabili ikiwa ni shamrashamra ya maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike duniani, uliofanyika katika kijiji cha kulelea watoto yatima cha SOS Mombasa mjini Zanzibar.

Walisema ni vyema serikali ikaandaa utaratibu utakaowasaidia kutoa maoni yao juu ya kero na changamoto zinazomkabili mtoto wa kike na ili yafanyiwe kazi kwa uarahisi.

Walisema hatua hiyo itasaidia serikali kujua mahitaji wanayotaka watoto hao na kuandaliwa mazingira mazuri kwa ajili ya mustakabali mzima wa vizazi vya sasa na vijavyo.

Walifahamisha kwamba licha ya kwamba serikali kuendeleza juhudi na mikakatim ya kuwasaidia watoto hao lakini bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa hivyo kuwasilisha maoni yao kupitia chombo hicho itakuwa mkombozi wa kuondosha matatizo hayo.

“Licha ya kuwepo wasemaji wa watoto ndani ya chombo hicho lakini kupatiwa nafasi watoto hao kujisemea wenyewe itakuwa chachu ya kuisaidia serikali kupanga mipango yake kwa ufanisi na kuweza kuleta tija hapa nchini,” walisema.

Mbali na hayo watoto hao walitumia fursa hiyo kuiomba serikali kuangalia iwezekano wa kuondosha vigenge na maskani zilizokuwepo karibu na skuli ili kuweza kuwakinga watoto hao na vitendo vya udhalilishaji.

Kwa upande wa Mratibu wa Masuala ya Elimu kutoka skuli ya SOS Zanzibar, Evelyn Baruti, alisema ni vyema serikali kutengeneza sera rafiki kwa watoto ili waweze kuwa na fursa ya kuzitumia na kufahamu mahitaji yao mapema.

Alisema licha ya serikali kufanya jitihada kadhaa ya kuwasaidia watoto wa kike lakini bado kwa baadhi ya maeneo hayajaweza kutatuliwa.

Kwa upande wa Meneja wa Sera na Utetezi kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, (TAMWA) Zanzibar, Salma Amir Lusangi, alisema wameamua kushirikisha wanafunzi kutoa changamoto zao ili kubaini matatizo yanayowakabili watoto wa kike.