NA MWANAJUMA MMANGA

WATU wasiojulikana wamechoma moto banda la Retisia Joseph Shingela (39) mkaazi wa Tunguu Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Suleiman Hassana Suleiman, alisema tukio hilo limetokea huko Tunguu Kibondeni, Oktoba saba mwaka 2020, majira ya saa 10:00 usiku, ambapo watu hao walichoma moto akiwa mwenyewe amelala chumbani kwake ndipo aliposhtuka na kukimbia na kutoka nje.

Alisema baada ya kutoka nje mmiliki huyo alipiga kelele na majirani  zake walitoka na kumpa msaada wa kuzima moto huo, ambapo ndani ya nyumba alikuwa anakaa peke yake.

Alisema kuwa moto huo umeunguza vitu mbali mbali zikiwemo nguo kumi, pesa shilingi laki mbili, simu moja, aina ya Tecno na kusababisha hasara ya shilingi laki saba kwa kukisia.

Kamanda Suleiman, alisema hadi sasa bado watu hao hawajapatikana na jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi zaidi na watapowabaini hatua kali za kisheria zitachukuliwa.

Hivyo, aliwataka wananchi kuwa karibu na jeshi la polisi pale wanapohisi kama kuna mtu wamehitilafiana na mtu kuripoti mapema ili linapotokezea tukio lolote kuweza kusaidia polisi.