NA KAHAMIS SAID, AHWK

WATU wenye ulemavu nchini wametakiwa kutumia fursa za kiuchumi zilizopo katika mazingira wanayoishi ili kujikwamua na ugumu wa maisha.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa wilaya ya Kat, Unguja, Hamida Mussa Khamis alipokuwa akikabidhi msaada wa matufali 300 kwa kikundi cha ‘Na sisi tuwe mbele’ kilichopo shehia ya Mpapa, wilaya ya Kati Unguja kwa ajili ya ujenzi wa panda la kufugia kuku.

Alisema baadhi ya watu wa kundi hilo kukaa na kuacha kujishughulisha na shuhuli yoyote, hivyo aliwapongeza wanachama wa kikundi hicho kwa kujiunga pamoja na kujishughulisha mbali mbali ikiwemo ya kilimo na ufugaji.

Mkuu huyo wa wilaya aliwaahidi wana kikundi hicho kuwa serikali ya wilaya kwa kushirikiana na Baraza la mji la wilaya ya Kati, wataendelea kuwapatia mchanga na vifaa vyengine kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa banda hilo.

“Serikali na baraza letu la mji litaendelea kuwa karibu nanyi kuhakikisha lengo lenu la kuwa na mradi wa kujiendeleza kiuchumi linatimia na kuwaomba watu wengine wenye ulemavu kuacha kukaa kando bali wajiunge katika vkundi kama hivi,” alisema DC Hamida.

Mapema mwenyekiti wa kikundi hicho, Mwachoum Vuai Hassan alimshukuru mkuu huyo wa wilaya kwa kuwapatia msada huo na kuomba kupatiwa mchanga ili kukamisha ujenzi wa mabanda mawili yatakayokuwa na uwezo wa kuchukua kuku 200.

Kikundi cha ushirika wa Watu wenye ulemavu ‘Na sisi tuwe mbele’, kimeanzishwa mwaka mwaka 2011 kwa lengo la kuondokana na utegemezi kina wanachama wanane, wakiwemo wanawake watano na wanaumme watatu.

Wakati huo huo, Mkuu huyo wa wilaya amekabidhi kompyuta tano kwa skuli ya Umoja Uzini zilizotolewa na Mfuko wa Mawasiliano kwa wote Tanzania kwa ajili ya wanafunzi wa somo la kompyuta katika skuli hiyo.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo skulini hapo Hamida aliwataka walimu na wanafunzi kuthamini   na kutunza misaada wanayopatiwa kutoka kwa wahisani mbalimbali ili kuongeza ufanisi katika kujifunza.

“Mwalimu Mkuu nakuomba usimamie matumizi ya komyuta hizi uwe ni kwa ajili ya kujifunzia kwa sasa wakati tukiendelea kutafuta misaada Zaidi ili vijana wetu wajifunze kwa ufanisi zaidi,” alisema DC Hamida.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwalimu Mkuu wa skuli hiyo Mohammed Masoud Mohammed, alisema msaada huo ni faraja kwa walimu na wanafunzi wa skuli na kuomba kupatiwa baadhi ya programu za kufundishia katika darasa la komputer katika skuli hiyo.