NA   ARAFA MOHAMED

BARAZA la Manispaa Mjini limeanza kutumia sheria za papo kwa papo,  kwa atapatikana anachafua mazingira kwa makusudi, kwa kulipishwa shilingi 30,000 ikiwa ni hatua itayosadia kupunguza tatizo la utupaji taka ovyo.

Ofisa Uhusiano Baraza la Manispaa Mjini, Seif Ali Seif, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na Zanzibar Leo, Ofisini kwake Malindi Mjini Unguja, ambapo alisema taasisi hiyoimejipanga kudumisha usafi wa mazingira katika mji hasa katika majengo mapya yaliofunguliwa hivi karibuni likiwemo jengo la Thabit Kombo.

Alisema, katika kuhakikisha mji unakuwa safi muda wote wameboresha mpango kazi wa usafishaji wa maeneo yote, ili mji uwe katika hali nzuri yakuvutia kwa kushirikiana na kampuni mbalimbali za usafi.

Aidha Seif alisema kuwa, kampuni nyingi za usafi zimejitokeza kwa ajili ya kushiriana na Baraza la Manispaa katika suala zima la usafi ili kuhakikisha wanaondoa uchafu katika maeneo hayo yaliopo Kisonge.

Alieleza miongoni mwa mikakati hiyo ni kudumisha siku ya kufanya usafi utakaofanyika kila baada ya mwezi mmoja ambayo itakua endelevu.