NA MWAJUMA JUMA NA ASYA HASSAN

WAWAKILISHI wateule wa majimbo ya Uzini, Chwaka na Tunguu wilaya ya Kati Unguja, kupitia Chama cha Mapinduzi CCM, wamesema watasimamia ilani ya chama hicho ili kutatua kero zinazowakabili wananchi wao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hilo, walisema wameomba nafasi hizo ili kuweza kuwatumikia wananchi, hivyo watazitumia ili wasijutie uwamuzi wa kuwachaguwa wao.

Mwakili wa Jimbo la Chwaka, Haji Issa Ussi alisema aliomba ridhaa katika CCM na amechaguliwa, hivyo kazi kubwa atakayoifanya ni kufanya yale ambayo yameainishwa katika ilani ya chama chake 2020/2025.

“Mimi nimechaguliwa na Chama cha Mapinduzi, na CCM imeelekeza yote yatakayotekelezwa kwenye ilani yake ambayo ndio nitakayoifata ili kutatua changamoto za wananchi”, alisema.

Kwa upande wake mwakilishi wa Jimbo la Uzini, Haji Shaaban Waziri alisema wananchi watambuwe wamechaguwa mtu wa kumtuma katika kutekeleza mambo mbali mbali ya maendeleo ndani ya jimbo hilo.

Hivyo alisema kwa kuwa yeye ni daraja lililounganisha baina ya wananchi na Serikali hatorudi nyuma kuyatekeleza yale ambayo aliwaahidi katika kipindi cha kampeni.

Mwakilishi huyo mteule alisema katika kuona vijana wanakuwa na ajira zao binafsi bila kutegemea serikalini watawapeleka vijana hao katika vyuo vya amali ili kujifunza kazi mbali mbali za mikono.

Akizungumzia kina mama alisema kuwa wataanzisha SACCO’S ya Uzini na kuwaingizia mtaji ambao utatumika kwa ajili ya kuanzisha biashara ndogo ndogo za ujasiriamali  ili waweze kujiunuwa kiuchumi.

 Hivyo alisema kuwa ili kuona Jimbo lao linakuwa na maendeleo chochote kile ambcho watakuwa wanawapatia wananchi wao hawatoingilia na watakuwa wakijisimamia wenyewe.

“Sisi tumechaguliwa ili tuwatumikie wao, kwa hiyo tutakuwa tukiwapa msukumo wananchi wetu kwa kuwatatulia kero mbali mbali ili waendelee kutuamini”, alisema.