NA ABOUD MAHMOUD

MPAKA katika miaka ya karibuni ilikuwa kawaida kukutana na mtoto wa miaka sita au saba njiani wakati jua ndio kwanza likianza safari yake ya kila siku ya kutoka mashariki kwenda magharibi.

Safari hio ya kilomita mbili hadi tatu kutoka nyumbani ni ya kwenda skuli kutafuta elimu ya dunia na baada ya masomo, huku jua likiwa kali au mvua ikiwa inanyesha.

Shida hii iliwaumiza sana watoto na kuwasononesha wazazi huku wakiingojea siku ya kujengewa skuli karibu na eneo lao ili masafa marefu ya kwenda na kurudi skuli yawe sehemu ya historia ya eneo lao.   

Hatimaye Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kwa kulitambua tatizo hili, imefanya juhudi kubwa na hasa katika miaka ya hivi karibuni  imefanikiwa kuwapunguzia watoto na wazee wao dhiki hii kwa kujenga skuli katika kila eneo lililo karibu na wananchi.

Hivi sasa takriban maeneo mengi  ya mji na vijiji yanayo skuli shemu za karibu na imewapunguzia wanafunzi machofu ya muda mrefu wa kwenda na kurudi skuli.

Katika awamu ya saba ya serikali iliyoongozwa na Rais Ali Mohammed Shein juhudi zaidi za kufikia lengo hilo zimeoonekana na kwa kuzingatia uhaba wa ardhi baadhi ya skuli zilizojengwa ni za ghorofa na kuwekewa vifaa vinavyohitajika kwa masomo.

Watu wa Zanzibar wanapaswa kuipongeza kwa kuwasogezea  watoto wetu huduma hii muhimu ya maisha na zaidi kwa kuipata bila ya malipo, tafauti na ilivyokuwa siku za nyuma, hali iliyopelekea wanafunzi wengi kushindwa kuendelea na masomo.

Hata hivyo, kumekuwepo tatizo ambalo jamii inahitaji kulifanyia kazi ili kuepusha matatizo mbali mbali yanayojitokeza na yatakayoweza kujitokeza kwa watoto wetu siku za mbele .

Katika orodha hii ya matatizo ni pamoja na wazazi na walezi wengi wanapohama eneo moja kwenda jengine kutowafanyia uhamisho wa skuli watoto wao. Hii imepelekea baadhi ya watoto kukatisha masomo.

Wazazi wengi ambao huwaandikisha watoto wao katika skuli zilizopo katika maeneo ya mijini mara baada ya kuhama kimakaazi na kwenda  maeneo mengine huwa hawajali kuwatafutia watoto wao skuli za karibu na hapo walipohamia.

mwanafunzi,

Yapo matatizo mengi yanayomkabili mwanafunzi, hususan katika madarasa ya kwanza mpaka la tano. Nalo ni la kuchelewa kufika skuli,mahudhurio madogo baadhi ya skuli, utoro, kudhalilishwa na madereva na utingo wa gari za abiria kuwadhalilisha na hata kuwabaka.

Kinachosikitisha ni wakati mwengine utaona utingo anawadhalilisha wanafunzi na hata kuwapiga mateke wasiingie kwenya gari, lakini wazazi waliomo ndani ya gari hukaa kimya badala ya kuwasaidia hao watoto. Wanasahau ukimlinda mtoto wa mwenzako na wa kwako atalindwa.

Suala la utoro linashamiri kwa sababu wazazi wengi hawana tabia ya kufuatilia maendeleo ya masomo ya watoto wao.

Hili tatizo la utoro linaweza kuleta athari kubwa kwa jamii kwani wanapotoka nyumbani huaga kwenda skuli na mwisho wake hawafiki na hawajulikani wapi wanapokwenda.