NA HUSNA SHEHA

MWALIMU Mkuu Msaidizi wa skuli ya msingi Kibweni, Khadija Ali Sleiman, amewataka wazazi na walezi wameombwa kushirikiana na walimu ili kuona wanafunzi wanafanya vizuri katika mitihani yao ya taifa.

Alitoa ombi hilo wakati wakati akizungumza na Zanzibar leo, ambapo alisema umoja na ushirikiano wao utaweza kupandisha kiwango cha ufaulu wa michipuo kwa wanafunzi wao katika mitihani ya taifa inayotarajia kufanya Desemba 14, mwaka huu.

Aidha alisema mwaka huu walimu wanamatumaini makubwa ya kupasisha wanafuzi wengi kutokana na muamko wao, na ari waliokuwa nayo ingawa wanakabiliwa na changamoto mbali mbali katika masomo yao.

Mwalimu huyo, alibainisha kwamba licha ya kuwa  na vipindi vya kawaida vya masomo pia wamepangiwa vya ziada ,ili kuwajenga vizuri wanafunzi wao katika masomo yao.

Sambamba na hayo alisema katika skuli hiyo jumla ya wanafunzi 571 wanatarajia kufanya mitihani wakiwemo 182 wa darasa la sita na 389 wa darasa la nne.

Hata hivyo, mwalimu huyo amewataka wazazi na walezi wazidishe ushirikiano na walimu, sambamba na kuwafuatilia nyendo zao na masomo yao.

Hata hivyo, alisema skuli yao inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa madarasa na uhaba wa walimu.

Husna Hemed Masoud, Mwanafunzi anaesoma katika skuli hiyo alisema watajitahidi kwa kadiri ya uwezo wao, ili wafanikiwe kufaulu michipuo na kuweza kufika elimu ya juu.