NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Riziki Shemdoe, kufika kwenye kiwanda cha maziwa kinachojegwa kihanga Karagwe, ili kutatua changamoto anazozipata Mwekezaji wa kiwanda hicho.

Waziri Bashungwa, ametoa maagizo hayo jana  alipotembelea na kukagua ujenzi wa kiwanda cha kuchakata maziwa cha Kahama Fresh kinachojengwa eneo maalum la viwanda lililopo Kihanga, wilaya ya Karagwe, Mkoa Kagera.

“Namuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara kufika hapa Kihanga Karagwe kwenye kiwanda cha maziwa kinachojengwa, akiambatana na Idara ya Maendeleo ya Viwanda na taasisi za NARCO, TIC, EPZA, TARDB, TANESCO pamoja na taasisi nyingine Katibu Mkuu atakazoona Zinafaa kumsaidia mwekezaji ili kuhakikisha kiwanda hiki hakikwami” amesema Bashungwa

Waziri Bashungwa, amepongeza jitihada za mwekezaji mzawa wa Kahama Fresh Limited, Jossam Mtangeki, kwa kusaidia utekelezaji wa dira Serikali ya awamu ya tano katika ujenzi wa uchumi wa viwanda maana kwa mkoa hapakuwa na kiwanda cha maziwa chenye ukubwa wa kuchakata lita 10,000 kwa siku.

Sambamba na hayo, Waziri Bahungwa amefurahishwa na mpango wa uwekezaji ambapo kutakuwa na kiwanda kinachotengeneza vyakula vya ng’ombe wa maziwa pia amepongeza kwa kuwepo kwa shamba la ngo’ombe wa mfano ambalo linawasaidia wafugaji wadogo wadogo kupata elimu ya ufugaji.

Aidha, Waziri Bashungwa amejadiliana na mwekezaji  mpango wa kugawa ngo’ombe kwa wafugaji wadogo wadogo na namna ya kuwasaidia ili kupitia Serikali, Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara na wizara ya Kilimo ziweze kuwaweka katika mfumo wa ushirika.