KHADIJA KHAMIS, MAELEZO

WAZIRI wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed amewashukuru wafanyakazi wa Wizara hiyo kwa mashirikiano waliyompa katika kipindi chake cha uongozi. 

Aliyasema hayo wakati wa hafla ya kuagwa na wafanyakazi wa wizara hiyo huko Mnazimmoja, alisema mashirikiano ya wafanya kazi ndio njia pekee iliyomsaidia kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi

Aidha aliwataka wafanyakazi hao kuendeleza mashirikiano yaliyopo katika utendaji wa kazi zao ili kuweza kutekeleza kazi zao kwa weledi.

Akitoa nasaha kwa wafanyakazi hao alisema katika ufanyaji wa kazi zao waepukane kuekeana chuki kwani chuki huzalisha uadui katika sehemu za kazi.

“Binaadamu anatakiwa awe msatahamilivu na awasamehe wenziwe wanaomkosea, kwani kufanya hivyo kutasaidia upendo na maelewano kazini hivyo nawaomba msipendelee kuzalisha maadui katika kazi zenu,” alisema Waziri.

Aliwataka wafanyakazi hao kujiepusha na masuala ya siasa wakati wa kazi pamoja na kutorudia makosa ya mara kwa mara katika utendaji wa kazi hizo.

Aliwataka kufanyakazi kwa kujiamini na kuwa na msimamo wakati wanapotekeleza majukumu yao. kuachana na msongo wa mawazo wakati wa kuwahudumia wagonjwa kwani kufanya hivyo kutahatarisha maisha ya watu.

Akisoma hotuba ya naibu waziri wa wizara hiyo Harusi Ali Suleiman, Naibu Katibu wa Wizara ya Afya Halima Maulid, alimshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa kumuamini waziri huyo kwa kumpa nafasi ya uongozi katika wizara hiyo.

Aidha aliwashukuru wafanyakazi wa wizara hiyo kwa kuwa pamoja nae kwa kumuunga mkono, kumpa ushauri pamoja na mashirikiano ambayo yalimpa ujasiri wa kuiongoza wizara hiyo

Nae Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya Dk. Fadhil Abdala, alitoa shukrani kwa viongozi hao kwa niaba ya wakurugenzi wenzake kwa ustahamilivu, utulivu na ushupavu wa viongozi hao, uliowawezesha kupambana na majukumu yao hasa wakati wa kipindi cha vita Corona.

Alieleza katika kipindi cha uongozi wao waliweza kuunganisha wafanyakazi wote kuwa kitu kimoja bila ya ubaguzi jambo ambalo limeunganisha wafanyakazi kuwa na mashirikiano mazuri katika kazi zao

Nae Afisa Mdhamini, kutoka Pemba Shadya Shaaban Seif, akitoa neno la shukurani kwa viongozi hao ambao wamemaliza muda wao wa utumishi katika kipindi hichi, aliwapongeza kwa ushauri na mashirikiano yao makubwa katika kazi.

Alisema viongozi hao waliweza kuwapa moyo na hamasa pamoja na uweledi wa kutekeleza majukumu ya kazi zao kwa lengo la kuwahudumia Wagonjwa kwa ufanisi mkubwa.