BISHKEK,KYRGYZSTAN

WAZIRI  Mkuu wa Kyrgyzstan,Kubatbek Boronov amejiuzulu,baada ya maandamano ya nchi nzima kupinga matokeo ya uchaguzi wa bunge.

Nafasi ya Boronov, mshirika wa Rais Sooronbay Jeenbekov ilizibwa na Sadyr Japarov,mwanasiasa mzalendo ambaye waandamanaji walimuachia huru kutoka gerezani siku moja kabla.

Maandamano hayo ya ghasia yalisababisha mtu mmoja kufa na watu wengine 700 kujeruhiwa.

Ghasia hizo ziliisababisha Tume ya Uchaguzi ya Kyrgyzstan kuyafuta matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika Jumapili iliyopita.

Upinzani nchini humo ulisema umechukua madaraka ya nchi hiyo, baada ya kuyavamia majengo ya serikali.

Dmitry Peskov, msemaji wa Rais wa Urusi, Vladmir Putin alisema nchi hiyo ina wasiwasi kuhusu ghasia hizo.

Wakati huo huo, Marekani,ilitoa wito mzozo huo wa Kyrgyzstan kusuluhishwa kwa njia ya amani na watu kujizuia na ghasia.