BANGKOK,THAILAND

WAZIRI Mkuu wa Thailand Prayut Chan-ocha amesema Serikali yake inajiandaa kuondoa hali ya dharura jijini Bangkok mapema iwapo hakutakuwa na matukio ya vurugu.

Alitoa maoni hayo kwenye hotuba yake kwa njia ya televisheni, ambapo Serikali ilitangaza hali ya dharura jijini Bangkok mnamo Oktoba 15 ambayo ilipiga marufuku mikusanyiko ya watu zaidi ya watano.

Maandamano makubwa yamekuwa yakifanyika ndani na nje ya jiji kuu la nchi hiyo kwa siku nane mfululizo kuanzia Oktoba 14.

Waandamaanji wanataka kujiuzulu kwa waziri mkuu na mabadiliko kwenye ufalme.

Vijana waliandamana jirani na ofisi ya waziri mkuu, kwenye chuo kikuu na kwingineko na kusababisha msuguano na kundi la waandamanaji wanaotaka kuulinda ufalme.

Waandamanaji wanasema Serikali iliwatia nguvuni viongozi wao chini ya hali hiyo ya dharura.

Kwenye hotuba yake iliyorushwa kwa njia ya televisheni, Prayut alidai kwamba waandamanaji walibeba vifaa vya chuma na utumiaji wa mizinga ya maji wa polisi hautofanya kuwa na jamii bora.

Waziri mkuu huyo aliashiria kufanyika kwa kikao cha bunge kisicho cha kawaida ili kujadili hatua za kuchukua kuhusiana na maandamano hayo.