NA NASRA MANZI

MKUU wa Mkoa Kusini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud, ameziomba taasisi za kibenki nchini kuwekeza katika miradi ya maendeleo ili wananchi wanufaike na huduma zao.

Akizungumza na viongozi wa serikali, taasisi za kidini na viongozi wa kamati za maendeleo katika ofisi ya mkoa huo Tunguu kikao kilichoandaliwa na benki ya NMB kwa ajili ya kujadili maendeleo ya mkoa huo.

Alisema endapo taasisi hizo zitaekeza katika miradi hiyo itasaidia kupunguza umaskini na kuinua uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.

Hata hivyo, alisema maendeleo pamoja   na kuhitaji ardhi, watu na uongozi bora, lakini bado kunahitajika mitaji kwa ajili ya kuendeleza shughuli hizo ambazo zinafanyika kulingana na wakati.

Ayoub alizitaka taasisi za kidini kuhamasisha waumini kufungua akaunti ili kusudi kutunza fedha zao, ili zibaki katika hali ya usalama, sambamba na kukuza hali ya kiuchumi kulingana na mabadiliko ya mifumo ya sayansi na teknolojia.

Mkurugenzi wa benki NMB Zanzibar, Abdalla Duchi, alisema benki hiyo imeanza kuboresha huduma mbali mbali kwa wateja ikiwemo NMB kiganjani mwako, huduma za bima pamoja na mikopo yenye riba nafuu ili kuona kwamba huduma zao zinanufaisha wananchi na taifa.