NA ZUHURA JUMA, PEMBA

WAZAZI nchini wametakiwa kuacha tabia ya kuwafungia ndani watoto wenye mahitaji maalumu, badala yake wawapeke skuli ili wapate haki yao ya elimu.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Abdalla Mzee Abdalla, katika kongamano la siku ya walimu lililofanyika Ukumbi wa Baraza la Mji Chake Chake Pemba.

Alisema, elimu ndio msingi wa maisha ya mwanadamu, hivyo ni vyema kuwapeleka skuli watoto hao, ili kuwawezesha kujiletea maendeleo katika maisha yao ya baadae.

“Mufanye jitihada kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalumu wanakwenda skuli, wala musiwafiche kwani itakuwa hamuwatendei haki”, alisema Naibu huyo.

Aidha Naibu Katibu huyo aliwataka walimu kujenga mikakati ya kuwafikia watoto wanaohitaji elimu mjumuisho, ili waweze kufanikisha vyema masomo yao kama walivyo watoto wengine.

Mkurugenzi wa Jumuiya inayohusika na Makuzi na Maendeleo ya Mtoto (Madrasa Early childhood program Zanzibar) Khamis Abdalla Said alisema, wanaendelea na mradi wa elimu mjumuisho ambao unalenga kuwajengea uwezo walimu kupata elimu hiyo, itakayowasaidia wakati wa kufundisha.

“Ni mradi wa miaka mitano na umejikita kwa Wilaya ya Chake Chake tu kwa Pemba, tunaendelea kuwapatia elimu mjumuisho walimu mbali mbali, ili kuwajengea uwezo na kuwapa ujuzi wa kuwafundisha watoto wenye mahitaji maalumu”, alisema Mkurugenzi huyo.