LUSAKA,ZAMBIA

SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) limetadharisha juu ya ongezeko la watu wanaokumbwa na matatizo ya kisaikolojia barani Afrika, kutokana na athari hasi za janga la corona.

Matshidiso Moeti, Mkurugenzi Mkuu wa WHO katika eneo la Afrika alisema janga la corona limeongeza mgogoro wa afya ya kiakili barani humo,kutokana na namna lilivyovuruga hali ya kiuchumi na kijamii ya nchi za bara hilo.

Alibainisha kuwa,kutengwa (karantini), kupoteza ajira, kuwapoteza wapendwa, pamoja na wimbi la taarifa zinazohusu virusi vipya (vya corona) kunaweza kuongeza kiwango cha msongo wa mawazo na kusababisha matatizo ya kisaikolojia, au hata kuwazidishia mashaka wenye matatizo hayo.

Alisema janga la ugonjwa wa Covid-19 linakumbusha umuhimu wa kuwekeza katika mfumo wa afya ya akili Afrika, bara ambalo lina nchi 15 kati ya 30 zinazoongoza kwa kesi za watu kujitoa uhai duniani.

Moeti alisema viongozi wa nchi za bara hilo wanapaswa kuushughulikia kwa udharura mgogoro wa afya ya akili ambao ulipuuzwa kwa miaka mingi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa WHO katika eneo la Afrika, utafiti uliofanywa hivi karibuni nchini Afrika Kusini ulionyesha kuwa, asilimia kumi hadi 20 ya watu 220 waliohojiwa wanasema janga la corona limewazidishia wasi wasi, sonona na msongo wa mawazo.

Aidha wanawake 12,000 walioshirikishwa katika utafiti mwengine uliofanywa katika jamii za watu wenye kipato cha chini huko Uganda na Zambia walisema mgogoro wa corona uliwasababishia sonona, hofu na msongo wa akili.