KINSHASA,DRC

SHIRIKA la Afya Duniani WHO limetangaza kuwa, limechukizwa mno na madai ya wafanyakazi wake ya kujihusisha na vitendo vya unyanyasaji wa kingono katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Shirika la WHO lilisema katika taarifa yake kwamba,linachunguza madai hayo ya vitendo vya unyanyasaji wa kingono vilivyofanywa na wafanyakazi wake dhidi ya wanawake zaidi ya 50 mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya congo wakati wa kukabiliana na janga la Ebola kati ya mwaka 2018 hadi 2020.

Baadhi ya wanawake hao waliwaambia waandishi wa habari kwamba, walifanyiwa vitendo hivyo na wanaume ambao ni wafanyakazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Ripoti zinasema kuwa,wanawake ambao hawakuwahi kuripoti visa hivyo vya ubakaji kwa kuhofia ulipizaji kisasi,wanawatuhumu wafanyakazi kadhaa wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali kuwanyanyasa kijinsia.

Wanawake hao walikuwa wapishi,na wengine walikuwa wakijihusisha na shughuli mbalimbali za usafi katika ofisi za mashirika hayo,na walikuwa wakilipwa kati ya dola 50 hadi 100 kwa mwezi.

Ikumbukwe kuwa,huko nyuma pia kuliwahi kutolewa ripoti inayoonyesha kuwa,wanawake katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo walikuwa wakilazimika kufanya ngono mkabala wa kupewa chanjo ya ugonjwa hatari wa Ebola, ambao uliua mamia ya watu hadi sasa.