NA MWANDISHI WETU

SHIRIKA la Afya la Kimataifa (WHO), limekabidhi msaada wa vifaa vya zaidi ya shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuendeleza mapambano dhidi ya ‘corona’.

Msaada huo ni pamoja na mashine 30 za Oxygen, vifaa vya upasuaji na mashine 12 za kupimia chlorine.

Akikabidhi msaada huo, Mwakilishi wa WHO Zanzibar, Dk. Andermichael Ghirmay, alisema, umelenga katika kuendeleza mapambano ya maradhi ya ‘corona’ licha ya kupungua kwake huku kukiwa na tishio la maambukizi mapya kwa baadhi ya mataifa.

Alisema, WHO itaendelea kushirikiana na Serikali ya Zanzibar katika kuhakikisha hali za afya za wananchi na wageni wanaoingia zinabakia salama kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Akipokea msaada huo, Mkurugenzi wa Wizara ya Afya, Dk. Jamal Adam Taib, alisema, Wizara ya Afya inaendelea kuwafuatilia wageni na wenyeji kwa ajili ya kuhakikisha nchi inabakia salama kwa maambukizi mapya ya ‘corona’.

Alisema, vifaa hivyo ambavyo kwa kiasi kikubwa vitasaidia kwa njia moja au nyengine na mapambano hayo yanayoendelea dhidi ya corona.

“Kwa kiasi kikubwa wananchi wamepata elimu juu ya kujikinga na ‘corona’, lakini, bado tunatakiwa kuendelea na vita hivyo”.

Aidha, alisema, serikali imezindua mpango wa kutokomeza kipindupindu huku jitihada kadhaa zilikichukuliwa ikiwa ni pamoja na uchimbaji wa mitaro na usambazaji wa maji safi na salama.

Hivyo, alisema, wizara imejipanga kutoa chanjo hasa katika maeneo hatarishi yanayokumbwa mara kwa mara na maradhi hayo.

Alisema, chanjo ya kipindupindu ‘dozi’ 60 tayari zipo kwa ajili ya kuanza kutumika katika maeneo hayo, lengo likiwa ni kutokomeza kipindupindu Zanzibar.