“Nilionewa kwa jinsi niivyoonekana, wenzangu shuleni walinidhihaki kwa majina ya utani kama “ng’ombe” na ‘pundamilia’, uonevu ulikuwa mbaya mpaka nililazimika kuacha masomo na kuwa mwanafunzi nyumbani.”
Huyo ni mwanamitindo kutoka nchini Canada, Winnie Harlow anaetambulika sehemu nyingi ulimwenguni kwa urembo na upekee kwenye tasnia ya mitindo.


Winnie Harlow amezaliwa Julai 27, 1994, huko Greater Toronto, mwenye asili ya Jamaika, ambae ni mtoto wa Lisa Brown na Windsor Young, pia ana dada wawili.
Wakati akiwa na umri wa miaka mine mrembo huyo aligundulikana na maradhi sugu ya ngozi yanayotambulika kama ‘vitiligo’, ambayo ngozi huwa na mabaka meupe maeneo tofauti ya mwili na kuendelea kuambukizika.


Haikua rahisi kwake kuikubali hali hiyo, kwani wenzake walimcheka na kumdhihaki kwa kumwita majina mabaya tofauti kama ng’ombe,pundamilia n.k.
Unyanyasaji kutoka kwa wanafunzi wenzake, ulimfanya abadilishe shule mara kadhaa, ilifika hatua hata kufikiria kutaka kujiua kutokana na kuchoka kuvumilia udhalilishaji huo, hivyo ilimbidi kuacha shule.
“Kuacha shule ya sekondari lilikuwa jambo bora kwangu kwa sababu nilipata hali ya kujifurahisha, nilijifunza kupenda nilivyo, hii ilinipa ujasiri wa kusimama imara kwenye kikwazo chochote maishani mwangu”.alisema Winnie wakati wa mahojiano yake na CNN


Kama waswahili wasemavyo ‘Mungu hakupi kilema akakukosesha mwendo’, hivyo licha ya changamoto mbali mbali za kimaisha kutokana na hali ya ngozi yake, hivi sasa amekua ni mfano mkubwa kwa watu wengi duniani wanaopenda tasnia hii ya urembo na wanamitindo.
Baada ya maisha ya mateso mengi aliyopitia, muonekano wa ngozi yake ndio iliomfanya awe mwanamitindo wa kipekee ulimwenguni, hata kwa wale waliomcheka na kumdhihaki hivi sasa wamekua mashabiki zake wakubwa.


Ijapokua haikua ndoto ya Winnie kuwa mwanamitindo, kwani alitamani kuwa mwandishi wa habari wa burudani, ila alijiingiza kwenye tasnia ya mitindo, na jamii ilimkubali na wengi walimuunga mkono.
Kupitia tasnia hiyo, Winnie alipata nguvu na ujasiri wa kusimama na kuionesha dunia nini maana ya kujikubali, kujiamini jinsi ulivyo, na pia alitoa maana ya uzuri wa kweli.


Winnie amefanya kazi na kampuni nyingi za kimataifa za mitindo kama ‘Victoria’s Secret Fashion Show’, pia kuonekana kwenye kurasa za mbele za majarida mashuhuru ulimwenguni miongoni mwao ni jarida la ‘Vogue’.


Pia, kutokana na umahiri na uthubutu wake kwenye mitindo na mambo ya kijamii amepata tuzo tofauti miongoni mwao ni tuzo ya ‘Beauty Idol’ katika jarida la Ujerumani, kwenye tuzo za ‘Gala’s Spa Award’ ya mwaka 2015.


Mbali na mitindo, yeye pia ni msemaji na mtetezi mkubwa wa umma, kwa kushajihisha jamii kujikubali jinsi walivyo, kwani hivyo huwafanya wao kuwa wakipekee, pia kuwavutia wengine kutambua kwamba uzuri huja katika maumbo, ukubwa, na rangi tofauti.
Mnamo mwaka 2016, Winnie alikuwa miongoni mwa wanawake 100 wa BBC yaani ‘BBC’s 100 Women’, ambapo alikua ni mmoja ya waliochaguliwa na BBC kwenye orodha yake ya wanawake wenye hamasa na ushawishi kwa mwaka 2016.


Mrembo huyo pia ameonekana kwenye video mbali mbali za muziki za waimbaji tofauti kama ‘Lemonade’ ya Beyonce na ‘Guts Over Fear’ ya Eminem.
Winnie aliwahi kuwa na mahusiano ya kimapenzi na Muimbaji wa kimarekani Wiz Khalifa, kwa sasa ana mahusiano na Kyle Kuzma, mcheza mpira wa kikapu mashuhuri wa ‘Los Angeles Lakers’.


Mwanamitindo huyo ambae alikata tamaa na maisha kutokana na kutengwa na kudhalilishwa, hivi sasa ni kipenzi cha wengi duniani, kwani ana zaidi ya wafuasi 8,000,000, katika ukurasa wake wa Instagram.
Hadithi ya mwanamitindo huyu, ni mfano mkubwa wa kuigwa, ambao utabadili mitazamo ya watu, kwa kuwakubali wenye muonekano tofauti, kuwa vyovyote walivyo huo ndio uzuri wao, na wanaweza kuleta maendeleo kwenye tasnia tofauti.


“Nina furaha na ngozi yangu, na naona fahari jinsi nilivyo, mimi kuvaa uhalisia wangu ni ujasiri mkubwa” Winnie
Utofauti wako ndio uzuri wako, jiamini, jikubali, simama na uioneshe jamii kuwa umebarikiwa uzuri wa kipekee.