NA TATU MAKAME

WIZARA ya Afya Zanzibar imesema inatarajia kujenga nyumba za wafanyakazi katika Hospitali ya Wilaya Kivunge Mkoa wa Kaskazini Unguja, ili kuondosha changamoto inayoweza kujitokeza ikiwemo kukosa wafanyakazi nyakati za usiku.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Ofisini kwake Mnazi mmoja, Mkurugenzi Idara ya Tiba Wizara ya afya Zanzibar, Dk. Juma Salum Mbwana (mambi) alisema ujenzi wa nyumba hizo zinatarajiwa kujengwa kupitia bajeti ya mwaka 2020-2021.

Alisema ujenzi huo, utaanza kwa jengo la ghorofa tatu zenye familia sita kwa hatua ya awali, ikiwa ni hatua iyayosababisha wagonjwa kupata tiba kwa wakati wote, ikiwa ni hatua itayoondoa kero kwa wenye mahitaji maalum hasa nyakati za usiku.

“Tutaanza na jengo lenye familia chache na baadae kuendelea na nyumba nyengine dhamira ya serikali kuendelea kusogeza huduma karibu hivyo kujenga nyumba kutafikia azma ya serikali ya kutatua kero kwa wananchi”,alisema..

 Akigusia kuhusu wazazi wanaokwenda kujifungua katika Hospitali ya Kivunge, DK. Mambi, alisema changamoto za wazazi zimetatuliwa kwa kujengewa jengo la mama na mtoto lenye kutoa huduma zote.