NA MWAJUMA JUMA

Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wanawake na Watoto kwa kushirikiana na Kijiji cha kulelea Watoto SOS, wamesema  watazidisha kuwapa elimu itayowasaidia watoto walioondokewa na wazazi wao na wale wenye mazingira magumu kwa lengo la  kuwaepusha na udhalilishaji.

Akizungumza na Wananchi wa Shehia ya Donge  Kipange Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mratibu wa Mradi wa Malezi Mbadala, Nyezuma Simai Issa, amesema watoto wanahitaji usimamizi na ulinzi katika malezi ili wapate mahitaji yao muhimu ya kibinadamu.

Amesema yapo mahitaji muhimu ambayo watoto wakiyakosa kunauzekano mkubwa wa kufanyiwa udhalilishaji hivyo wazazi wajikubalishe kupatiwa chakula, malezi bora, elimu, na malazi.

Hata hivyo Nyezuma, amewataka wazazi na walezi kuwashuhulikia watoto ili kuwaepusha na vitendo vya udhalilishaji ambavyo  hurudisha nyuma maendeleo na ustawi wa mtoto katika makuzi yake.

Ofisa Ustawi wa Jamii Kaskazini ‘A’ Makame Makame Haji,

amesema bado vitendo vya udhalilishaji na ukatili kwa watoto vipo katika Mkoa wa kaskazini Unguja  ambavyo vinarudisha nyuma ustawi wa Watoto ambapo  kupitia Mradi wa Malezi Mbadala  utawawezesha wazazi na walezi kuibua matukio na vitendo vya udhalilishaji dhidi ya watoto.

Amesema hatua kali zitachukuliwa kwa watendaji wa matukio ya udhalilishaji endapo wananchi wataweza kuwafichua wanaotenda matendo maovu kwa watoto kwa kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Wakitoa  sababu za udhalilishaji  kwenye shehia yao  Wananchi wa Donge Kipange  wamesema   wapo baadhi ya wazazi wanawapiga watoto wao hadi kupelekea kuwazalilisha jambo ambalo husababisha mtoto kupata ulemavu wa viungo kutokana na kipigo wanachokipata kwa wazazi wao.