NA NASRA MANZI
WIZARA ya Vijana, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar imesema itachangia shilingi 3,000,000, kwa ajili ya kusaidia mashindano ya Yamle Yamle cup yanayoendelea hivi sasa.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara hiyo Omar Hassan ‘King’, wakati akizungumza na viongozi pamoja na wanamichezo hivi karibuni, kwenye dimba la Mao Zedong Kikwajuni.
Alisema Wizara itajitahidi kusimamia na kuratibu shughuli za michezo ili kuleta ari na hamasa katika uibuaji wa vipaji kwa vijana.
Hata hivyo aliwataka vijana kuendelea kupenda michezo na kuachana na vikundi ambavyo havitakuwa na tija katika jamii.
King aliwataka wanamichezo kuendelee kuwa na nidhamu kwa viongozi wao,ili kufikia malengo waliokusudia katika maisha yao.
Alieleza kuwa licha ya kuwepo kwa uhaba wa wafadhili lakini Serikali ya awamu ya saba ilijitahidi na kuhakikisha michezo inaendelea kwa kutatua changamoto zilizopo ili kukuza vipaji kwa vijana na michezo nchini.
Kwa upande wake mgombea wa nafasi ya Uwakilishi jimbo la Kikwajuni Nassor Salim Aljazeera, aliwataka wafanya biashara kuunga mkono na kusaidia michezo mbali mbali.
Sambamba na hayo aliwataka washiriki wa mashindano hayo pamoja na mashabiki kuendelea kudumisha amani na kujiepusha viashiria vinavyoweza kuleta vurugu.