NA KHAMISUU ABDALLAH

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar inatarajia kuzifunga skuli zote za serikali na binafsi na kusikitisha kambi kwa muda wa wiki moja ili kupisha uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Katibu mkuu wa wizara hiyo, Idrissa Muslim Hija alieleza hayo wakati akizungungumza na Zanzibar Leo ofisini kwake Mazizini nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Alisema wizara itazifunga skuli hizo kuazia Oktoba 24 mwaka huu na kuzifungua Novemba 2 ili kulinda usalama wa wanafunzi katika kipindi hicho, pia kutoa fursa ya majengo ya skuli kutumika kwa shughuli za uchaguzi.

Dk. Muslim alitaja sababu nyengine zilizolazimisha kufungwa kwa skuli hizo ni kutokana na kuwa takriban wasimamizi na watendaji wengi wa uchaguzi huo ni walimu kutoka skuli mbalimbali.

“Agizo hili halitawahusu wanafunzi wanaosoma vyuo vikuu kwani vyuo hivyo vina taratibu na sheria zake, pia tukisema watoto waende skuli watakwenda katika mazingira gani na matayarisho yataanza kufanyika kabla ya siku ya uchaguzi,” alisema Dk. Muslim.

Akizugumzia madai ya wazazi wa wanafunzi wanaofanya mitihani kuwa watoto wao watakusa muda wa matayarisho ya mitihani, alisema wiki moja haiathiri na kwamba wanapaswa kuwasimamia kudurusu masomo yao wakiwa nyumbani.

Alisisitiza kuwa ni vyema kwa skuli zilizoanzisha kambi katika kipindi hicho kuzifunga mara ili kuepusha muingiliano wa wanafunzi na watu wengine ambao wanaweza kuathiri mfumo wa kujifunza.

“Wazazi wanaona mtoto anasimamiwa skuli tu ili aweze kusoma bila ya kufahamu kwamba nasi tunajukumu la kuhakikisha tunawasimamia katika kudurusu masomo yao wakiwa nyumbani,” alisisitiza.

Mbali na hayo Dk. Muslim aliwasisitiza wamiliki wa skuli binafsi kuhakikisha wanafuata maelekezo yaliyotolewa na serikali kwani wapo kwa mujibu wa sheria.

“Serikali inapotoa uamuzi wake basi wafahamu inakaa na kujadili na kuona uzito wa suala haikurupuki, hivyo ni vyema skuli binafsi kufuata taratibu tunazozielekeza kwani wiki moja sio kubwa watarudi skuli na kuendelea na masomo”, alisema.

Uchaguzi mkuu wa rais, wabunge, wawakilishi na madiwani unatarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu ambapo kwa uchaguzi wa Zanzibar utatanguliwa na kura ya mapema itakayopigwa Oktoba 27.