NA MWANDISHI WETU

BIASHARA ya utalii ni moja kati ya biashara zinazokuwa kwa kasi ulimwenguni ambapo katika mwaka 2018 pekee, jumla ya watalii bilioni 1.4 walitembelea sehemu mbalimbali ulimwenguni ikiwa ni ongezeko la asilimia 6 ikilinganisha na mwaka uliopita.

Kwa mujibu wa Shirika la Utalii Ulimwenguni (UNWTO) katika kipindi hicho cha mwaka 2018, kumekuwa na ongezeko la watalii waliotembelea maeneo yote duniani ambapo huko Mashariki ya kati watalii waliongezeka kwa asilimia 10, Afrika asilimia 7, Asia, Pasifiki na Ulaya asilimia sita kila eneo na Amerika kulikuwa na ongezeko la asilimia 3.

Jumla ya watalii 713 milioni walitembelea barani Ulaya katika kipindi hicho cha 2018 ambapo wengi walitembelea kusini na kati mwa bara la Ulaya. Wengine walifanya matembezi yao katika mashariki na kati mwa bara la Ulaya huku eneo la kusini mwa ulaya na ukanda wa bara hilo wenye kupakana na bahari ya Mediterenia ukipokea wastani wa asilimia 7 ya watalii wote walotembelea Ulaya.

Hata hivyo idadi ya watalii waliotembelea kaskazini mwa Ulaya ilipungua kutokana na kushuka kwa kiwango cha watalii waliotembelea Uingereza kutokana na Brexit.

Watalii 217 milioni walitembelea eneo la Amerika ambalo linajumuisha Amerika ya Kaskazini, Amerika ya Kusini, Amerika ya kati pamoja na visiwa vya Caribbean.

Kwa upande wa bara la Afrika, watalii 67 milioni walitembelea bara hilo ambapo kaskazini mwa Afrika kulikuwa na ongezeko la asilimia 10 ya watalii na kusini mwa Jangwa la Sahara kulikuwa na ongezeko la watalii la asilimia 6.  Eneo la Mashariki ya kati lilirikodi watalii milioni 64.

Pamoja na mambo mengine kuongezeka kwa idadi ya watalii waliotembelea maeneo mbalimbali ulimwenguni kumechangiwa na mambo kadhaa. Baadhi ya sababu hizo ni pamoja na jinsi mataifa yanavyojitangaza kupitia mawasiliano ya mitandao, kuwepo kwa urahisi wa safari za ndege, meli na ardhini zinazorahisisha usafiri kati ya bara na bara.

Baadhi ya makampuni makubwa yanayokusanya Mabilioni ya Dola ulimwenguni kila mwaka kutokana na biashara ya utalii ni pamoja na Tui, Carnival Corporation, Marriot International, Accor Hotels, Booking.com, Expedia na Airbnb.

Tui Group Travel  yenye Makao Makuu yake nchini Ujerumani ndiyo kampuni yenye kuongoza duniani kwa mapato makubwa ya biashara ya utalii. Kampuni hiyo yenye matawi katika nchi 180 ulimwenguni pia ina mawakala 1600 wa kusafirisha watalii duniani, kampuni sita za ndege zenye ndege 150, hoteli mia tatu na meli 17 za kutembeza watalii. Mapato ya kampuni hiyo yenye wafanyakazi 71, 413 hapo mwaka 2018 yalikuwa ni Dola Bilioni 1.56.

Carnival Corporation ni kampuni kubwa kabisa duniani inayomilikiwa na wawekezaji kutoka nchini Uingereza na Marekani. Kampuni hiyo yenye Makao Makuu yake huko Doral, Florida nchini Marekani ina jumla ya meli kubwa kumi za kifahari za kutembeza watalii na meli nyengine za wastani mia moja ambazo hutembeza watalii katika maeneo mbalimbali uliwmenguni.

 Kampuni kadhaa tanzu za usafirishaji watalii kwa meli zinazomilikiwa na kampuni hiyo ziko katika nchi mbalimbali zinazotembelewa na watalii wengi kwa meli duniani.

Baadhi ya meli hizo za kifahari zinazotembeza watalii ni pamoja na zile zilioko huko Hong Kong nchini China, Rostock nchini Ujerumani, Genoa, Italia pamoja na Sydney nchini Australia. Meli nyenginezo za kifahari za kampuni hiyo ziko Marekani na Uingereza. 

Kampuni hiyo iliyoajiri wafanyakazi 120,000 ilikusanya Dola Bilioni 2.99 mwaka jana kutokana na kusafirisha watalii kwa kutumia meli zake za kifahari. Marriot International ni kampuni ya kitalii inayomiliki na kuendesha jumla ya hoteli za kifahari  milioni 7 duniani kote.

Kampuni hiyo yenye Makao Makuu yake katika mji wa Bethesda huko Maryland nchini Marekani. Marriot International ina jumla ya wafanyakazi 176,000 duniani kote ambapo mwaka juzi ilikusanya wastani wa Dola Bilioni 1.90 kutokana na biashara hiyo ya mahoteli.

Kutokana na uwezo mkubwa wa kifedha wa kampuni hiyo, imezinunua kampuni kadhaa maarufu duniani na kuziingiza katika umiliki wake. Baadhi ya kampuni kubwa zilizonunuliwa na kampuni hiyo ya Marriot International ni pamoja na kampuni ya mahoteli ya Starwood Hotels ya nchini Marekani ambayo ilinunuliwa kwa Dola Bilioni 13 hapo mwaka 2015.

Mwaka huo huo wa 2015, Marriot International iliinunua kampuni ya Delta Hotels ya Canada iliyokuwa ikimiliki mahoteli ya kifahari 38 nchini Canada. Kampuni nyengine kubwa duniani inayovuna mamilioni ya fedha kutokana na biashara ya utalii ni Accor Hotels yenye Makao Makuu yake katika mtaa wa Sequana Tower mjini Paris nchini Ufaransa. Kampuni hiyo inamiliki hoteli 4,800 za madaraja mbalimbali katika jumla ya nchi mia moja duniani kote.

Kampuni hiyo imeajiri wafanyakazi 280,000 ulimwenguni ambapo katika miaka ya hivi karibuni kampuni hiyo, imefungua mahoteli kadhaa huko kusini mashariki mwa bara la Asia kutokana na kuongezeka kwa watalii wanaotembelea  eneo hilo. Katika mwaka 2018 kampuni hiyo ilikusanya wastani wa Euro Bilioni 2.284 kutokana na biashara hiyo.

Booking.com ni kampuni maarufu ulimwenguni inayopokea kwa njia ya mtandao maombi ya safari za kitalii kwa watalii mbalimbali duniani. Kampuni hiyo ni mkusanyiko wa kampuni mbalimbali za kitalii ambapo mwaka 2018 ilipokea jumla ya maombi 97.2 Milioni ya watalii waliotaka kusafiri sehemu mbalimbali duniani.

Kampuni hiyo ilianzishwa mwaka 1996 mjini Amsterdam nchini Uholanzi na inapokea maombi ya huduma za usafiri na malazi kwa watalii katika lugha 43. Huduma za kampuni hiyo zinatolewa kupitia mitandao mbalimbali na hivyo kurahisisha upatikanaji wa wateja. Mwaka 2018, kampuni hiyo ilikusanya jumla ya Dola Bilioni 3.918.

Expedia ni kampuni nyengine ya kitalii inayotoa huduma kwa njia ya mtandao ambayo inakusanya mamilioni ya fedha kutokana na biashara hiyo.  Kampuni hiyo yenye Makao Makuu yake huko Seattle nchini Marekani  inapokea maombi ya huduma za usafiri wa aina zote na malazi  kwa  watalii  wanaotembelea sehemu mbalimbali ulimwenguni.

Kampuni hiyo imeajiri jumla ya wafanyakazi 24,500 na ilikusanya  dola 377.9 Milioni  hapo mwaka 2017.

AIRBNB ni kampuni nyengine ya kimtandao ambayo inapokea  huduma za  maombi ya safari za kitalii, nyumba za kupumzikia na  malazi. Mwaka jana wastani wa  wateja  Milioni 500 kutoka maeneo mbalimbali duniani waliomba huduma za kampuni hiyo.

Kampuni hiyo yenye Makamo Makuu yake katika jiji la San Francisco huko California, Marekani imeajiri wafanyakazi 12,736 ambapo mwaka 2017 ilikusanya Dola 93 Milioni. 

Hata hivyo kutokana na dunia kuathiriwa na maradhi ya Corona, pato la utalii duniani linatarajiwa kuporomoka ambapo inakisiwa kuwa jumla ya Dola Trilioni moja za utalii zitapotea kutokana na maradhi hayo ulimwenguni kote.

Moja ya meli ya kifahari inayomilikiwa na kampuni ya kitalii ya Carnival Corporation