NA MWANDISHI WETU

YANGA SC wametoka nyuma na kushinda mabao 2-1 dhidi ya wenyeji, KMC katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.

Kwa ushindi huo, mabingwa hao wa kihistoria, wanafikisha pointi 19 katika mchezo wa saba, ingawa wanabaki nafasi ya pili, nyuma ya vinara, Azam FC waliokusanya pointi zote 21 katika mechi saba, wakati mabingwa watetezi,Simba SC ni wa tatu kwa pointi zao 13 za mechi sita.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Ramadhan Kayoko aliyekuwa anasaidiwa na Hamisi Chang’walu na Abdul Malimba wote wa Dar es Salaam KMC, walitangulia kwa bao la Hassan Salum Kabunda dakika ya 27.

Kabunda, mtoto wa beki wa Yanga SC miaka ya 1990, Salum Kabunda, sasa marehemu alimtungua kipa Metacha Boniphace Mnata kwa shuti kali la umbali wa mita 22 baada ya kuwahadaa walinzi wa Yanga kufuatia kupokea pasi ya kiungo mwenzake, Kenny Ally Mwambungu.

Kiungo Tuisila Kisinda kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akaisawazishia Yanga SC kwa mkwaju mzuri wa penalti dakika ya 41 akimchambua kipa mkongwe Juma Kaseja kufuatia mshambuliaji Mghana, Michael Sarpong kuangushwa kwenye boksi.

Kipindi cha pili, Yanga SC wakafanikiwa kupata bao la ushindi kupitia kwa mshambuliaji wake mpya, Waziri Junior aliyemalizia kwa kichwa kona ya mtokea benchi Farid Mussa Malik dakika ya 61.

Baada ya kufunga bao hilo, Waziri, alivua jezi kuonyesha fulana iliyoandikwa ‘The King of CC Kirumba Stadium’, akimaanisha yeye ni Mfalme wa Uwanja huo kutokana na rekodi yake ya mabao, tangu akiwa anachezea Toto Africans na Mbao FC zote za Mwanza ambazo zimeshuka Daraja.

Mechi nyingine za Ligi Kuu, Biashara United imeshinda 1-0 dhidi ya wenyeji, Polisi Tanzania bao pekee la Deogratius Judika Mafie dakika ya 53 Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara.