NA MWANDISHI WETU

KISIWA cha Yelibuya kipo kaskazini magharibi ya Sierra Leone huko Afrika Magharibi, kikiwa na wakaazi wapatao 5,000.

Kwa muda sasa wakaazi wengi wa kisiwa hicho wamelazimika kuhama kutokana na kuanza kuzama kidogo kidogo kwa kumezwa na mafuriko ya maji ya Mto Kolente unaomwaga maji katika bahari kuu ya Atlantiki.

Kisiwa cha Yelibuya kina urefu wa maili 32 na upana wa maili 15. Kwa miaka kadhaa wakaazi wa kisiwa hicho ambacho kimezungukwa na msitu mkubwa wa mikoko wamekuwa wakikata mikoko hiyo kwa ajili ya kujengea nyumba za kuishi na kupikia.

Hatua hiyo imetokana na ukweli kwamba kisiwa hicho hakina huduma ya umeme na aina nyengine ya nishati mbadala na hivyo kuwalazimisha wakaazi hao kukata mikoko kwa matumizi hayo.

Mbali ya hayo pia kutokana na ukosefu wa umeme, wavuvi wengi wa kisiwa hicho hawana vifaa vya baridi vya kuhifadhia samaki na hivyo hukausha samaki wao kwa kutumia kuni ambazo ni miti ya mikoko.

Kuongezeka kwa kina cha maji kila uchao, kuliwafanya wakaazi hao walazimike kukata mikoko ili kujengea nyumba mpya katika maeneo mengine ya kisiwa hicho kwa vile nyumba za mwanzo ziliingia maji na hivyo kulazimika kuhama.

Kina cha maji kimekuwa kikiongezeka kila uchao ambapo ufukwe wa bahari unaozunguka kisiwa hicho umekuwa ukididimia kila uchao na hivyo kuyafanya maji ya bahari kusogea katika makaazi ya watu.

Mbali ya ukataji huo wa mikoko kuwa ni chanzo kimoja wapo cha kuongezeka kwa kina cha maji katika kisiwa hicho, lakini pia kutokana na kuongezeka kwa joto duniani, kina cha maji ya bahari kimekuwa kikiongezeka siku hadi siku.

Mbali ya kuwa ni mazalia ya samaki na viumbe wengine wa baharini, lakini mikoko iliyozunguuka kisiwa hicho ilikuwa ni kizuizi cha maji ya bahari na ilipunguza kasi ya kina cha maji kuingia ardhini.

Msitu wa mikoko nchini Sierra Leone unachukua asilimia 47 ya ufukwe wa bahari wa taifa hilo ambapo kuna wastani wa hekta 183,789 za msitu huo.

Mikoko hiyo inapatikana pembezo mwa Mto Kolente, Mto Sierra Leone, katika ghuba na upwa wa magharibi ya nchi hiyo na katika ghuba ya Yawri na pembezo ni Mto Sherbro.

Lakini kutokana na kukatwa kwa kasi kwa miti hiyo kwa muda mrefu na kuacha wazi eneo kubwa linalozunguka kisiwa hicho bila kizuizi, ndipo maji ya bahari yalipopata nafasi ya kuingia ardhini hadi majumbani.

Ingawa hakuna takwimu halisi za ukubwa wa kiwango cha maji ya bahari yaliyoingia kisiwani humo, lakini wazee wengi walioishi kisiwani humo kwa zaidi ya miaka 50, wamethibitisha kuwa maji ya bahari yalianza kuingia kidogo kidogo kisiwani humo kiasi miaka 30 iliyopita.

Wataalamu wengi wa mazingira na wanasayansi wanakubaliana kuwa iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa kuzuia hali hiyo, kisiwa hicho kitaondoka katika ramani ya dunia katika kipindi cha miaka 20 ijayo.

Kuongezeka kwa kiwango hicho cha maji katika makaazi ya watu katika kisiwa cha Yelibuya kumeongeza kasi ya ukataji wa mikoko kwa ajili ya majenzi ya nyumba mpya na kuni. Kinyume chake hali hiyo inaongeza wigo wa maji yanayopanda ardhini. 

Kijografia, kisiwa cha Yelibuya ni kiungo muhimu kinachounganisha  mji mkuu wa Sierra Leone, ambao ni Freetown na mji mkuu wa Guinea ambao ni Conakry. Baadhi ya wafanyabiashara wanaotumia njia za mkato hutumia kisiwa hicho kama kituo cha mapumziko baina ya miji mikuu miwili hiyo.

Kisiwa cha Yelibuya ni maarufu kwa uvuvi wa samaki na kilimo cha mpunga ambapo wafanyabiashara kutoka bara husafiri kwa njia ya bahari hasa kwa kutumia madau na mitumbwi kwenda kisiwani humo.

Wafanyabiashara hao hubadilishana na wakaazi wa kisiwa hicho samaki na mpunga kwa bidhaa nyenginezo kama vile nyugu nyasa, mboga ya kisamvu, nguo na zana za ujenzi.

Mbali ya ukosefu wa umeme na maji ya mfereji, lakini pia maji na bidhaa zote nyenginezo muhimu huingizwa kisiwani humo kutoka nje.

Wakaazi wengi kisiwani humo ambao wamekuwa wakiishi hapo kwa vizazi na vizazi wamekuwa katika hali ngumu ya maisha na kishindwa kuhama kutokana na ukweli kwamba wengi hawajui wapi pa kwenda na wamekuwa wakiishi hapo na familia zao.

Mbali ya hayo, pia wakaazi hao wanashindwa kuhama kwa vile wanamiliki mali zisizohamishika. Kutokana na sababu za kijografia kisiwa hicho kimekuwa kama kituo cha biashara.

Sierra Leone ni moja ya mataifa kadhaa duniani yaliyoathirika vibaya kutokana na mabadiliko ya tabia nchi ambapo mafuriko pamoja na maporomoko ya ardhi yamekuwa ni majanga ya kawaida nchini humo.

Katika mwaka 2017, zaidi ya watu 1000 walifariki mjini Freetown nchini humo baada ya kutokea maporomoko ya ardhi.

Waalamu wengi wa mazingira wanakubaliana kuwa pamoja na mambo mengine kudidimia kwa kisiwa cha Yelibuya ni matokeo ya uharibifu wa mazingira wa muda mrefu ulofanywa na wakaazi wa kisiwa hicho.

Wanamazingira hao wanasisistiza kuwa kung’olewa na kukatwa kwa msitu wa mikoko ulozunguka kisiwa hicho kwa muda mrefu kumesababisha ardhi kukosa kizuizi na hivyo kushindwa kuzuia maji kupanga ardhini na kuathiri maakazi ya binaadamu.\

Eneo la katikati la makaazi ya watu katika kisiwa cha Yelibuya yakiwa yameanza kudidimia kutokana na kuingia maji ya bahari.

https://www.aljazeera.com/mritems/Images/2018/8/14/c169f56668dd406c877c93e0dfc60ef3_18.jpg

Samaki  waliokaushwa katika kisiwa cha Yelibuya wakisuri wateja kutoka nje ya kisiwa hicho.