NA LAILA KEIS

CHAMA cha Walimu Zanzibar (ZATU) kimeitaka wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kutoa ushirikiano kwa chama hicho ili waweze kutatua changamoto zinazowakabili walimu hali itakayowawezesha kutekeleza vyema majukumu yao.

Katibu mkuu wa ZATU, Mussa Omar Tafurwa, aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari, katika kutoa tamko la kuelekea maadhimisho ya siku ya walimu duniani ambayo huadhimishwa Oktoba 5 kila mwaka.

Alisema, katika moja ya fursa wanayoipata katika kuadhimisha siku hiyo ni kutoa changamato za walimu, hivyo changamoto kubwa kutoka kwenye chama hicho ni kukosa mashirikiano mazuri kutoka kwenye wizara hiyo.

“ZATU ni chama pekee kinachoshughulikia masuala ya walimu nchini, lakini jambo la kusikitisha wizara ya elimu haitupi mashirikiano ya kutosha kwenye mambo ya msingi yanayowahusu walimu”, alisema Tafurwa.

Alifafanua kuwa wizara imeshindwa kuwashirikisha hata kwenye mipango ya utekelezaji wa kazi wakati wa janga la maradhi ya corona.

Katika hatua nyengine alisema, katika kuadhimisha siku hiyo, kila mwaka ZATU huandaa shughuli tofauti kama mikutano na waandishi wa habari, makongamano na maandamano ya walimu.

Lakini alisema, maadhimisho ya mwaka huu yameshindikana kufanyika maandamano, kutokana na shughuli za uchaguzi, lakini shughuli nyengine zinaendelea kama kawaida.

Hivyo alisema, itakapofika siku ya maadhimisho, kutakua na kongamano maalumu na mada itakuwa ni kuelezea mafanikio ya miaka 10 ya Dk. Shein.

Siku ya walimu duniani, huadhimishwa na walimu duniani kote, kwa kupitia vyama vyao, wakishirikiana na wadau wa elimu, ambao hufanya shughuli za ushawishi, utetezi na kampeni, lengo likiwa ni kumuwezesha mwalimu kutekeleza wajibu wake kikamilifu.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Walimu wanabeba mzigo, kwa kutengeneza hatma njema ya baadae”