NA LAYLAT KHALFAN

SHIRIKISHO la vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC), limesema lina matumaini mgombea wa urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi kufuatia ahadi yake ya kushughulikia changamoto zinazowakabili wafanyakazi nchini.

Khamis alieleza hayo hivi karibuni na kudai kuwa matumaini hayo yamekuja baada ya mgombea huyo kuzungumza na wafanyakazi kusikiliza changamoto zao mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil.

Miongoni mwa changamoto zilizoelezwa na wafanyakazi katika kikao hicho ni kupandishwa kwa kima cha chini cha mshahara kwa kuzingatia utaratibu wa mishahara kwa mujibu wa sekta za kiuchumi.

Khamis alitaja changamoto nyengine iliyoelezwa kuwa ni kurekebishwa mishahara ya mashirika ya umma ya mwaka 2019 ambapo baadhi ya mafao yaliyotolewa kwa mujibu wa sheria yalifutwa kwa wafanyakazi wa chini.

“Hili linaenda sambamba na marekebisho ya sheria ya ZSSF ambayo ni miongoni mwa athari kwa kupungua kwa kiinua mgongo kwa asilimia 40,” alisema katibu huyo.

Alisema majibu ya mgombea huyo ambae pia ni waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga taifa yamewapa faraja hasa alipowahakikshia wafanyakazi kuwa atatoa kipaumbele katika kusimamia haki na wajibu wa mfanyakazi.

“Ametutia moyo sana, na tunaamini kama akichaguliwa atatekeleza maneno yake kwani mfanyakazi hawezi kufanya kazi kwa bidii bila ya kupata maslahi yake au humuwezeshi kufanya kazi kwa umakini,” alisema.

Alisema iwapo kiongozi huyo atasimamia kikamilifu nidhamu, dhana ya kufanyakazi kwa mazoea itaondoka na watendaji watajirekebisha ili kuongeza upatikanaji wa haki zake za msingi.

Aidha Khamis alisema, Rais aliyepo tayari amefanya jitihada kubwa na kutoa maelekezo mengi kwa wafanyakazi juu ya kuboreshewa maslahi yao hususani wenye kazi nzito na za hatari lakini hakuna lililofanyika.

“Kwa vile mgombea wetu haya anayaelewa kwamba wapo viongozi ambao hawakubaliani na haya basi alihakikisha atakaowateua yeye maelekezo atakayoyatoa wanayafanyia kazi,” alisema.