NA LAYLAT KHALFAN
IMEELEZWA kuwa baadhi ya shehia za Makunduchi, mkoa wa Kusini Unguja, zinakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa muda mrefu.
Mkuu wa wilaya ya Kusini Unguja, Idrissa Kitwana Mustafa, aliyasema hayo alipokua akizungumza na mwandishi wa habari hizi kuhusiana na changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wilayani humo.
Aliyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na shehia ya Mzuri, Tasani, Kijini ambayo upatikanaji wa maji umekua ni wakusuasua ikilinganishwa na maeneo mengine.
Alisema hali hiyo licha ya kusababisha usumbufu kwa wananchi, pia hupelekea kutopatikana kwa huduma hiyo kwa wakati.
Idrissa alisema hali hiyo inasababishwa na uchakavu wa miundombinu ya maji ambayo ni ya muda mrefu jambo linalosababisha upungufu wa maji ndani ya shehia hizo.
Alisema ofisi yake imekuwa ikitoa taarifa mara kwa mara kwa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) lakini bado tatizo hilo linaendelea kuwepo bila ya kupatiwa ufumbuzi.
“Tulipowataarifu ZAWA kuhusiana na hili tatizo wanasema watalishughulikia lakini hadi leo bado linaendelea kuwaumiza wananchi wetu,” alisema.
Akizungumzia hali ya upatikanaji wa maji katika wilaya yake, Kitwana alieleza kuwa huduma ya maji safi na salama imefika asilimia 75 na kwamba maeneo machache ndio hayajapata huduma hiyo.