NA LAILA KEIS

TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), imewapa kipaumbele watu wenye ulemavu kwa kuwapatia vitambulisho maalumu vitakavyowawezesha kupiga kura kwa urahisi na mapema ili kuepukana na usumbufu.

Mkuu wa Divisheni ya Habari na Uhusiano wa Umma ZEC, Jaala Makame Haji, aliyasema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko ofisini kwake Maisara mjini Unguja.

Alisema, lengo la ZEC kwa kila uchaguzi kutoa vitambulisho hivyo ni kuwapa kipaumbele watu wenye ulemavu ili wasipoteze haki yao ya msingi kutokana na kuhofia usumbufu wa foleni na msongamano.

“ZEC tunatengeneza hivyo kwa kutekeleza sera ya jinsia na ushirikishwaji wa makundi ya kijamii ya mwaka 2015, ili kuwawezesha kupata huduma kwa urahisi na haraka”, alisema.

Aidha alisema, takwimu za watu wenye ulemavu ni takribani 4000, lakini ZEC pia ilizingatia umuhimu wa kuyapa kipaumbele mahitaji ya watu wenye mahitaji maalum mengine kama watu wazima, wajawazito na wanaonyonyesha.

Hivyo kwa ujumla ZEC imeandaa vitambulisho takribani 8000 na kuvigawa kila wilaya kupitia jumuiya zao ili viwafikie walengwa.

Jaala alisema, ZEC imetoa elimu kwa watendaji, mawakala, askari, pamoja na wasimamizi wote wa vituo, ili wafahamu umuhimu wa vitambulisho hivyo na kumpa kipaumbele yeyote watakaemuona na kitambulisho hicho.

Pia alisema, ili kuhakikisha vitambulisho hivyo vinawafikia walengwa, wanashirikiana kwa karibu na Idara ya Watu Wenye Ulemavu, ili kuhakikisha zoezi hilo linafikia lengo lililokusudiwa.

Akizungumzia vitambulisho hivyo, ofisa uhamasishaji Idara ya Watu Wenye ulemavu Zanzibar, Nurdin Kombo Hamadi, aliwataka watu wenye ulemavu kuitumia vizuri fursa hiyo, kwa kufika mapema siku ya kupiga kura wakiwa wamevaa vitambulisho hivyo.

Sambamba na hilo, aliwataka watu wenye ulemavu kuvitumia vizuri vipande hivyo, na mara tu baada ya kumaliza kupiga kura basi waviawache kituoni ili vije kufaa katika chaguzi zijazo.

Pia aliwataka wananchi pamoja na wasimamizi wa vituo vya kupigia kura, kuwapa kipaumbele watu wote wenye ulemavu hata kwa wale ambao hawatakuwa na vitambulisho hivyo.

Naye mmoja ya Watu wenye Ulemavu ambae tayari ameshapata kitambulisho hicho Abubakar Issa, aliishukuru serikali kupitia ZEC, kuwaandalia mazingira mazuri ya kupigia kura na kuwataka, wenziwe kujitokeza kwa wingi siku ya tarehe 28 kuwapigia kura viongozi wanaowataka.