NA LAILA KEIS

TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), imewataka wananchi wote waliojiandikisha na kuhakiki taarifa zao katika daftari la kudumu la wapiga kura, kufika kwenye vituo kuangalia majina yao na kujua vituo vyao vya kupigia kura.

Mkurugenzi wa Uchaguzi Zanzibar, Thabit Idarous Faina, aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika zoezi la ubandikaji wa daftari hilo huko skuli ya Mwembeladu Rahaleo mjini Unguja.

“Orodha iliyokuwepo kwenye daftari hilo ndio wanaopaswa kwenda kupiga kura Oktoba 28 mwaka huu na matarajio yetu kwa waliohakiki hakuna aliyekosekana kuorodheshwa”, alisema Mkurugenzi huyo.

Aidha alisema, waliojiandikisha kwa mujibu wa sheria ni wapiga kura 56,635, ambao wote wamo kwenye daftari hilo na wanatakiwa kufika kuhakikisha majina yao na kujua vituo vyao.

Katika hatua nyengine alisema, kwa wote ambao hawatokua na muda wa kufika vituoni, ZEC imeweka namba maalumu ‘USSD CODES’, *152*29#, ambazo mpiga kura atatakiwa kuingiza nambari ya kitambulisho cha kupigia kura na utamuwezesha kuona jina lake pamoja na kituo chake cha kupigia kura kupitia simu ya mkononi.

Hivyo aliwataka mawakala wa vyama vya siasa wafahamu kuwa daftari hilo ni kwa ajili ya matumizi ya mpiga kura si vyenginevyo, na serikali imetoa mifano 17 ya daftari hizo ambazo watapewa mawakala wa kila kituo ili waweze kujiridhisha.