NA JAALA MAKAME, ZEC

ZOEZI la upigaji kura wa mapema limeanza katika maeneo yote 407 yaliyopangwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ambapo idadi kubwa ya wapigakura waliohusika na walioomba kushiriki kupiga kura hiyo wamejitokeza vituoni kwa amani na utulivu.

Mkurugenzi wa Uchaguzi Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Thabit Idarous Faina wakati akitembelea katika vituo vya kupigia kura alisema, wapiga kura walijitokeza kwa wingi kutokana na Tume kujiandaa vizuri katika kufanikisha zoezi hilo.

Faina alisema zoezi hilo lipo kisheria na limewahusu wapiga kura maalum walioainishwa katika sheria ya uchaguzi nam.4 ya mwaka 2018 kifungu cha 82(2)(a)(b) na kuwaasa wale ambao hawakutajwa katika kifungu hicho kubaki nyumbani na badala yake wasubiri hadi tarehe 28 Oktoba, 2020.

Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa, kwa mujibu wa utaratibu wa kura ya mapema mawakala wa vyama vya siasa mara baada ya kukamilika upigaji kura wataweka lakiri zenye namba maalum katika masanduku ya kura ili kuhifadhi na kulinda usalama wa kura zilizopigwa.

Hata hivyo, Mkurugenzi Faina aliviasa vyombo vya habari vinavyoripoti matukio ya uchaguzi kutoripoti matokeo ya idadi ya kura zilizopigwa kwani mwenye jukumu la kufanya hivyo ni Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa upande wa Zanzibar.

Akizungumzia hali ya utulivu katika vituo vya kupigia kura Kamanda wa Mkoa wa Mjini Magharibi Awadhi Juma Haji aliwatoa hofu wananchi kuwa hali ya ulinzi na usalama imeimarika katika vituo vyote vya kupigia kura ambapo Jeshi la Polisi limejipanga kuendelea kuimarisha katika maeneo yote Zanzibar na kuwadhibiti wale wote wanaotaka kujaribu kuivuruga Amani iliyokuwepo nchini.

Nao, baadhi ya wapiga kura ya mapema waliofika vituoni kupiga kura walisema, utaratibu uliotumika kuendesha kura ya mapema ni mzuri na waliwasisitiza wananchi kuzifuata Sheria na taratibu zilizowekwa na Tume ili kufanikisha zoezi la Uchaguzi katika hali ya amani na utulivu.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inatarajia kuendesha upigaji kura wa pamoja leo  kwa wapiga kura waliomo katika daftari la kudumu la wapiga kura ambao hawakupiga kura ya mapema.