NA ASYA HASSAN

TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), imesikitishwa na kitendo kilichofanywa na baadhi ya watu kubandua majina ya wapiga kura yaliyobandikwa katika vituo mbalimbali vya Unguja na Pemba.

Mkurugenzi wa Tume hiyo, Thabit Idarous Faina, alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa ZEC uliopo Maisara mjini Zanzibar.

Alisema siku moja baada ya Tume hiyo kubandika majina ya wapiga kura yaliyomo kwenye daftari la kudumu la wapiga kura, hatimaye watu wasiojulikana wamepita katika vituo hivyo na kubandua.

Alisema Tume hiyo imepokea taarifa hiyo kutoka katika ofisi zake za wilaya Unguja na Pemba, kuwa baadhi ya vituo vya kupigia kura majina ya wapiga kura yamebanduliwa.

Alisema lengo la Tume hiyo kubandika daftari hilo ni kusaidia wananchi kuhakiki majina yao na kutambua vituo vyao vya kupigia kura.

Mkurugenzi huyo alisema kitendo kilichofanywa na watu hao si cha kiungwana na ni kosa kwa mujibu wa sheria za nchi.

“Tume inasikitishwa na kitendo kilichofanywa na baadhi ya watu hao, kwani daftari hilo si la tume bali limewekwa kwa ajili ya kuwaondoshea usumbufu wananchi pamoja na kujua vituo vyao vya kupiga kura,” alisema.

Hata hivyo Mkurugenzi Idarous alitumia fursa hiyo kuviomba vyombo vya ulinzi kuchukua hatua za haraka kwa lengo la kuwadhibiti watu hao, kutokana na hali hiyo inaweza kupelekea uvunjifu wa amani hapa nchini.

Sambamba na hayo alisema tume hiyo itakaa ili kuona njia sahihi watakazozitumia ili waweze kuwasaidia wananchi hao kupata haki zao za demokrasia.

“Ikiwa tume ipo katika kutafakari njia sahihi ya kuwasaidia wananchi hao ni vyema katika kipindi hichi kutumia namba ya simu ya zanteli ili waweze kupata taarifa hizo.

Akizungumzia hasara Mkurugenzi huyo, alisema kwa sasa bado mapema kujua hasara iliyopatikana kutoka na uharibifu huo.

Aidha alisisitiza wananchi ambao vituo vyao vipo salama ni muhimu kutoa mashirikiano ili daftari hilo liweze kubaki salama.

Akizungumza na gazeti hili, Kamishna wa Polisi Zanzibar, CP Mohammed Haji Hassan alisema jeshi lake limepokea taarifa hizo, hata hivyo bado mapema kuzitolea ufafanuzi na wanaendelea na uchunguzi.