NA JAALA MAKAME, ZEC
TUME ya Uchaguzi Zanzibar, inatarajia kupokea waangalizi wa Uchaguzi 50 kutoka katika taasisi za ndani ya nchi pamoja na za kimataifa.
Mkurugenzi wa Uchaguzi (ZEC) Thabit Idarous Faina, amesema hayo wakati akitoa mada juu ya matayarisho ya Uchaguzi Mkuu 2020, kwa Viongozi wa Dini kisiwani Pemba katika Ukumbi wa kiwanda cha mafuta ya Makonyo Wawi Pemba.
Alisema Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), tayari imeshafanya mambo mengi na kuchukuwa hatuwa mbali mbali juu ya mchakato wa uchaguzi ambazo zitawezesha kukamilisha uchaguzi huo kwa mafanikio makubwa.
Alisema Tume imeruhusu kuwepo kwa waangalizi wa Uchaguzi katika Uchaguzi Mkuu 2020, na jumla ya taasisi 61 za ndani ziliomba kupatiwa vibali na zilizokidhi vigezo ni 35.
Alifahamisha kuwa jumla ya taasisi 15 za kimataifa ambazo zimepatiwa vibali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC zimeomba pia kupatiwa kibali kuangalia Uchaguz wa Zanzibar.
Alifahamisha kuwa, miongoni mwa mambo hayo ambayo tayari yamekamilika ni uandikishaji wa wapiga Kura Wapya na uhakiki wa taarifa za wapiga kura ambapo jumla ya wapiga kura 566,352 waliandikishwa na wanatarajiwa kuwa Wapiga Kura katika uchaguzi mkuu wa 2020.
Aliendelea kueleza kuwa, Tume ya Uchaguzi imefanya uteuzi wa Wagombea 17 wa ngazi ya Uraisi wa Zanzibar, Wagombea 252 Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa majimbo mbali mbali ya Uchaguzi na Wagombea wa Udiwani 360 kwa Wadi zote.
Sambamba na hayo, pia Mkurugenzi alibainisha kuwa kwa mara ya Kwanza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetumia bajeti yote ya Uchaguzi kwa ukamilifu bila hata kutumia pesa za wafadhili.