NA ASYA HASSAN

TUME ya Uchaguzi ya Zanzibar, imesema ishaandaa mazingira rafiki na wezeshi katika vituo vya kupiga kura ili kuwasaidia watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali kuweza kupiga kura na kupata haki zao za kidemokrasia.

Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Hamid Mahmoud Hamid, alisema hayo alipokuwa akifungua mkutano kwa watu wenye ulemavu wa uziwi mkutano ambao ulifanyika katika Chuo cha Maendeleo ya Utalii kilichopo Maruhubi.

Alisema tume hiyo kazi yake ni kuhakikisha watu wote wanapata fursa kupiga kura, hivyo tayari zoezi hilo limeandaliwa ili kuona makundi hayo yanapata haki zao za msingi kama watu wengine.

Akitaja miongonj mwa mazingira waliyoyaandaa Mwenyekiti huyo alisema ni pamoja na kutoa vitambulisho maalum kwa ajili ya kuwatambua watu hao na kuwekwa wakalimani maluum kila kituo ili kuweza kuwasaidia.

Alifahamisha kwamba Zanzibar kuna jumla ya watu wenye ulemavu wa uziwi 1,268 na tume hiyo imeshachapisha vitambulisho 8,000 kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali Unguja na Pemba.

Aidha alitumia fursa hiyo kuyataka makundi hayo kujitokeza siku hiyo kwenda kuitumia haki zao ya kidemokrasia.

Hata hivyo, aliwasisitiza washiriki hao kuendelea kutimiza amani na utulivu katika kipindi chote cha uchaguzi na baada ya uchaguzi.

Mkurugenzi wa Tume hiyo Thabit Idarous Faina, alisema ZEC itaendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ili kuona zoezi hilo linafanyika kwa amani na utulivu.

Alisema hatua hiyo itasaidia kupunguza changamoto na malalamiko ya wananchi ambayo hujitokeza kabla, wakati na baada ya Uchaguzi.