NA ABOUD MAHMOUD

SHIRIKA la Umeme Zanzibar (ZECO) limeanza kufunga mita mpya ikiwa ni hatua ya kudhibiti vitendo vya wizi kwa lengo la ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na upotevu wa umeme ambao ulikuwepo hapo awali.

Akizungumza na Zanzibar Leo, ofisa mawasiliano wa ZECO, Haji Chapa, alisema mita hizo za ‘Split Meter’ zimeaanza kufungwa katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba ambapo wameanza katika nyumba za maendeleo.

Alisema tayari mita hizo zimeshafungwa katika nyumba za maendeleo Bambi, Gamba, Mpapa na Makunduchi kwa upande wa Unguja na hivi sasa wanaendelea katika nyumba za Michenzani na kwa upande wa Pemba wameanza na Chakechake na sasa wanaendelea katika maeneo mengine.

“Tayari shirika letu limeanza kufunga mita mpya katika maeneo ya nyumba za maendeleo na tumeingia katika maeneo mbali mbali yenye nyumba hizo kwa Unguja na Pemba kwa mjini na mashamba,” alisema.

Chapa alisema mbali na nyumba za maendeleo pia zoezi hilo kufunga mita mpya linafanyika katika maeneo ya viwanda pamoja na sehemu ambazo hawawezi kufikiwa kirahisi ikiwemo nyumba za ulinzi na usalama.

Afisa huyo alisema mara baada ya kumaliza katika maeneo hayo wataendelea na zoezi hilo katika mitaa mbali mbali ya nyumba za wananchi.

Alieleza kwamba maendeleo ya kiteknolojia ndio yanayofanya shirika lihamie upande huo kwa ajili ya kuwapa wananchi wake maendeleo yalio bora na huduma nzuri.

“Awali tulianzia na mita za kuzunguka ambazo wananchi walikuwa wanakuja kulipia umeme hapa, baadae tukatumia mita za kununua umeme na hivi sasa tunataka kuzibadilisha tuwe na hizi mpya kutokana na maendeleo yaliyopo kwa wakati uliopo,” alisema.

Hivyo Chapa alitoa wito kwa wananchi kutumia kwa uangalifu huduma ya umeme na kuachana na tabia ya kufanya hujuma ya miundombinu hiyo ambayo inaitia hasara serikali.

Alifahamisha kwamba mwananchi anapolifanyia hujuma shirika huwa anaifanyia serikali ambayo siku zote inahangaika kuwapelekea maendeleo wananchi wake.