NA MWAJUMA JUMA

SHIRIKISHO la soka visiwani Zanzibar (ZFF) linamatumaini makubwa ya kuona soka la wanawake linakuwa katika kushiriki michuano mbali mbali ndani na nje ya nchi.


Hayo yameelezwa na Katibu wa Shirikisho hilo Ali Ame Vuai katika hafla ya ufungaji wa mafunzo ya siku tano ya uongozi kwa wanawake kwa mpira wa miguu huko Amaan.


Alisema walikuwa na kiu kubwa ya viongozi wa mpira wa miguu kwa wanawake kupata mafunzo, ambapo kukamilika kwa mafunzo hayo kutaondosha changamoto hiyo.


Alisema uwepo wa viongozi wanawake utapelekea msukumo mkubwa kwa mchezo huo kuonekana kama ilivyo kwa wanaume.


“Kukamilika kwa mafunzo hayo kunatoa matumaini kwamba tutapata viongozi wa soka wanawake na kuuinua soka kwa wanawake”, alisema.


Akizungumzia kwa wale ambao walishindwa kuendelea na mafunzo,alisema wapo ambao walikosa uvumilivu na wengine walipatwa na matatizo nje ya uwezo wao ikiwemo maradhi.


Hivyo alisema kwa wale ambao walipata matatizo ya maradhi waliwasiliana nao na kuwaahidi kwamba wataingia mafunzo mengine ambayo yanatarajiwa kufayika kisiwani Pemba.


Mafunzo hayo ya siku tano yaliendeshwa na mkufunzi kutoka Shirikisho la Kimataifa la Soka FIFA Dk. Henry Tandao na kushirikisha viongozi wanawake 16 badala ya 30 walioteuliwa hapo awali.