NA ZAINAB ATUPAE

SHIRIKISHO la Soka Zanzibar (ZFF), limesema msimu huu limejipanga kuhakikisha wafanya mipango mizuri ili ligi iwe  nzuri na kuvutia.

Akizungumza na waandishi wa habari rais wa Shirikisho hilo Seif Kombo Pandu,alisema anaamini kuwa mipango hiyo itasaidia kutimiza malengo yao,ikiwemo kupata wadhamini watakao dhamini soka la Zanzibar.

Alisema viongozi wa shirikisho hilo wanaendelea kupambana,ili kuhakikisha msimu unaokuja ligi inakuwa nzuri na yenye thamani kama mashindano ya ndondo cup.

Aidha alisema kamati ya mashindano ya Shirikisho la Soka Zanzibar inayatambua mashindano ya Ndondo cup ambayo hufanyika visiwani Zanzibar baada ya kumalizika kwa ligi.

 Alisema mashindano hayo yanatambuliwa na yana kanuni zake kinachotakiwa kwa viongozi wanaoanzisha mashindano hayo kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa na kamati ya mashindano ya shirikisho.

 “Kanuni yetu inayatambua mashindano kama haya ambayo ni rasmi kwetu na yanaleta umoja,kujenga udugu na mshikamano,hivyo hatunabudi kuyaendeleza na kutoa mashirikiano kila yanapofanyika iwe Mjini au vijiji,”alisema.