NA ABOUD MAHMOUD

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) limeshauriwa kuwa na msimamo wa kutoongeza muda wa usajili, ili kuondosha tatizo la wachezaji kuchukuliwa bila utaratibu.

Akizungumza na Zanzibar Leo kocha mkuu wa klabu ya Real Kids, Khamis Abdulrahman ‘Amokach’, alisema utaratibu unaofanywa na ZFF, kuongeza muda  wa usajili mara kwa mara sio mzuri na unaathiri klabu zao ambazo zina hali duni.

Alisema kila inapofika muda wa usajili klabu hujipanga kwa kutafuta wachezaji ili waweze kuwa  nao katika kipindi chote cha ligi, lakini kitendo cha kuongeza muda kinaharibu  mipango ya klabu.

“Naishauri ZFF kukaa na kutafakari kwamba hili jambo la kuongeza muda mara kwa mara kwenye usajili linatuathiri sana sisi klabu ndogo,”alisema.

Amokachi alifafanua kwamba mara baada ya kukubaliana kusajili mchezaji na kuongezwa muda, mchezaji hupata vishawishi vya kuhama timu na uongozi huanza kusumbuka kutafuta mchezaji mwengine, baada ya kutokuwa na mikataba ya kuwazuwia kuondoka kama ilivyo madaraja mengine makubwa.

 Alisema kitendo hicho kinaziathiri klabu nyingi zenye uwezo mdogo hususan za madaraja madogo, ambayo wachezaji wake huwa rahisi kuchukuliwa.

Hivyo kocha huyo aliishauri ZFF kuiga mfano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ,ambapo linapoweka muda wa usajili huwa hauongezwi na hakuna tatizo linalotokea.