NA ASYA HASSAN

KITUO cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC), kimeeleza kuwa mradi wa ‘Jenga imani Tanzania’ unaandaa mazingira ya kupatikana wataalamu watakaosaidia kutatua migogoro ya wananchi pale inapotokea.

Mkurugenzi wa kituo hicho, Harusi Miraji Mpatani, alisema hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tatu kwa waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali, mafunzo, yaliyofanyika katika ukumbi wa kitengo cha kudhibiti Malaria, Mwanakwerekwe Zanzibar.

Alisema Zanzibar ni miongoni mwa nchi zinazopiga hatua ya maendeleo kupitia nyanja mbalimbali, hivyo hali hiyo imekuwa ikichangia uwezekano wa kutokea mambo yanayopelekea migogoro katika ngazi ya familia na jamii.

Alisema ili kukabiliana na matukio hayo, taasisi hiyo inasimamia mradi wa kujenga imani ya Tanzania, ambao utatoa mafunzo kwa taasisi za serikali na binafsi ili kupatikana wataalamu ambao watasaidia kutatua migogoro.

Alifahamisha kwamba lengo la kutoa mafunzo hayo ni kuwaandaa watu ambao watakuwa na uwezo na taaluma ya kutosha katika kutatua migogoro inayotokea ndani ya familia, jamii na hata katika maofisi.

“Mradi huu una uwezo mkubwa wa kusaidia kuchangia kuimarisha imani ya wananchi katika kujiepusha na migogoro tofauti ili nchi ibakie salama,” alisema.

Mkurugenzi huyo aliwataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao kuelimisha jamii juu ya mradi huo ili uwe chachu ya kuondoa migogoro katika jamii.

Mkufunzi wa mafunzo hayo, Omar Hamad Faki, alisema Zanzibar wapo wataalamu wengi wa utatuzi wa migogoro lakini mradi huo utaongeza nguvu ya kukabiliana na matatizo hayo kuepusha madhara au yasitokee.