NA HAFSA GOLO
MAMLAKA ya Usafiri Baharini (ZMA) imesema itashirikiana kikamilifu na vyombo vya ulinzi na usalama katika kipindi cha uchaguzi, ili kudhibiti uwingiaji wa watu kwenye bandari bubu zilizopo visiwa vya Zanzibar.
Meneja Uhusianao wa ZMA, Othman Said Othman, alieleza hayo alipokua akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Malindi.
Alisema utekelezaji wa zoezi hilo, umelenga kuisaidia serikali kuhusu uingiaji holela wa watu nchini, hasa kipindi cha uchaguzi, ambapo baadhi ya watu wanaweza kutumia mwanya huo kwa ajili ya kuharibu uchaguzi ama kuchochea vitendo vya uvunjifu wa amani.
Aidha, alisema ZMA itakuwa makini kwa kufanya ukaguzi katika maeneo yote ya bandari zisizo rasmin ambazo hutumiwa kwa ajili ya kusafirishia abiria na bidhaa nyengine zinazoingizwa nchini kinyume na utaratibu wa sheria.
Alifahamisha hatua hiyo itakuwa sambamba na kuwasaka abiria na wamiliki wa vyombo vya usafiri wa baharini wanaojikubalisha kusafirisha bidhaa za magendo kwa kutumia bandari hizo.