Waliojaribu kufanya fujo wadhibitiwa

NA WAANDISHI WETU

KWA mara ya kwanza Zanzibar imeendesha zoezi la kura ya mapema kwa amani hapo jana, zoezi ambalo liliwashirikisha wapiga kura walioainishwa katika kanuni na sheria, ambapo zoezi hilo litafuatia na upigaji wa kura wa pamoja utakaofanyika leo.

Zoezi hilo la kura ya mapema katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, limefanyika jana katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar huku hali ya amani ikitawala.

Licha ya kuwepo kwa hali ya wasiwasi katika baadhi ya maeneo ya mjini Unguja, zoezi hilo lilifanyika kwa kuhusisha watu mahsusi waliotajwa katika sheria namba nane ya mwaka 2020 ya uchaguzi Zanzibar.

Katika wilaya ya Magharibi ‘B’ zoezi hilo limekwenda vizuri baada ya wapiga kura kujitokeza kwa wingi katika vituo vilivyowekwa na Tume katika maeneo mbalimbali wilayani humo vikiwemo cha Mwanakwerekwe ‘C’, Kiembesamaki ‘A’ na Skuli ya sayansi ya Afya Mbweni.

Mkuu wa kituo cha Mwanakwerekwe ‘C’, Rashid Mwinyi Bakari alisema zoezi la upigaji kura limekwenda vizuri na wapiga kura walijitokeza kutumia haki yao.

Aidha mawakala wa vyama mbalimbali walishiriki kwenye aungalizi wa zoezi hilo la kura ya mapema na kuipongeza Tume kwa kuratibu vyema zoezi hilo.

Katika kituo cha skuli ya Kiembesamaki, mkuu wa kituo hicho Suleiman Idriss Shani, alisema hakuna mtu asiyehusika na uchaguzi huo aliyejitokeza na kwamba zoezi hilo limeenda vyema.

Akizungumzia mwenendo wa zoezi hilo, wakala kutoka chama cha ACT- Wazalendo, Khalfan Abdullah Khator, alisema upigaji wa kura umekwenda vizuri.

Katika Wilaya ya Mjini, zoezi hilo limekwenda vizuri baada ya wapiga kura kujitokeza kwa wingi katika vituo vilivyowekwa huku ulinzi ukiimarishwa baada ya kuwepo kwa dalili za watu waliopanga kulivuruga zoezi hilo.

Zanzibar Leo ilitembelea kituo cha kupigia kura kilichopo katika skuli ya Haile selassie, skuli ya Rahaleo, Mwembeshauri, skuli ya Dk. Ali Mohamed Shein na Miembeni kwa jimbo la Kikwajuni ilishuhudia makundi ya wapiga kura wakiwemo maofisa usalama na watendaji wa tume ya uchaguzi.

Msimamizi wa kituo cha Haile selassie Alhaj Daud Khamis, alisema zoezi hilo limekwenda vizuri na watu wamejitokeza kwa wingi kwa kila mwenye haki ya kupiga kura ya mapema.

Naye, Msimamizi wa uchaguzi jimbo la Kikwajuni Hashim Abrahman Swaleh alisema katika kituo cha Miembeni watu wamejitokeza kwa wingi.

Alisema katika kituo hicho hakuna mwananchi yoyote aliyejitokeza kupiga kura ambao hawamo katika daftari la kura ya mapema.