NA MARYAM HASSAN

WANANCHI wa Zanzibar wametakiwa kujitokeza kufanya uchunguzi wa afya zao wakati wa zoezi la uchunguzi wa maradhi mbali mbali linaloendelea katika viwanja vya Mnazi Mmoja mjini Zanzibar.

Wito huo umetolewa na Katibu wa taasisi ya Zanzibar Outreach Programme (ZOP) Dk. Naufal Kassim Mohammed alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo jana.

Alitaja maradhi yatakayochunguzwa kuwa ni shinikizo la damu, sukari na saratani ya matiti kwa wanawake na kwamba atakaebainika na viashiria vya maradhi hayo, atapatiwa matibabu mara moja.

Alisema katika kipindi hicho zaidi ya 600 ya wanawake wanatarajiwa kuchunguzwa ambapo katika siku ya jana watu 100 walijitokeza hadi majira ya mchana licha ya kuwepo kwa changamoto ya mvua.

Aidha Dk. Naufal aliwasihi wananchi kupunguza kula vyakula vya mafuta na vyakula vya makopo kwa sababu tafiti zimebainisha kuwa ndio chanzo cha saratani ya matiti.“Niwahahakikishie kuwa saratani hi inatibika pindi mtu akiwahi kuanza matibabu lakini matibabu yakichelewa madhara huwa makubwa,” alisema.

Kwa upande wa mjumbe wa kamati kuu ya ZOP, Mohammed Shaksy alisema zoezi hilo pia wanataraji kulifikisha maeneo ya vijijini ili kutoa elimu watu wengi zaidi.

Alisema kufanya hivyo kutarahisisha kupata idadi sahihi juu ya waliobainika na viashiria vya saratani ya matiti ambayo mpaka sasa inatibika.