Na Ali Othman

TAKRIBAN wiki mbili zilizopita Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), imezizindua nyumba za kisasa takribani 210, ikiwa ni mwendelezo wa sera ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kuwapatiwa makaazi bora na ya kisasa wananchi wake.

Sera hii ilitekelezwa kwa vitendo na aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar Hayati Mzee Abeid Amani Karume hasa kwa kuwa alijenga nyumba za makaazi katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba mijini na vijijini.

Kwa kuwa kila binaadamu ana haki ya kuishi na kuthaminiwa utu wake na jinsi yake, hivyo basi katika kukamisha ujenzi huo wa nyumba huko Mbweni, ni sehemu moja wapo ya kukusanya mapato ya taifa kwa ajili ya shughuli za  maendeleo ya nchi na watu wake kwa ujumla.

Ni vyema kwa serikali kupitia mfuko wa hifadhi ya jamii, kusimamia miradi kama hii mikubwa, kwa ajili ya kumpunguzia mwananchi mzigo mzito wa ujenzi wa nyumba hasa ukiangalia gharama za ujenzi zilivyo hivi sasa ukilinganisha na kipindi cha miaka 20 kilichopita.

Kwa kuwa Jamuhuri ya Tanzania kwa sasa ipo katika uchumi wa kati, hivyo ipo haja kupitia nyumba hizo za ZSSF iwe ni chachu ya kuendeleza uchumi na maaendeleo ya jamii kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Khamis Mussa, alieleza kwamba mradi wa nyumba hizo uligharimu jumla ya shilingi za Kitanzania bilioni 35, ambapo jumla ya majengo 10 yamekwisha kamilika.

Aidha katibu huyo alieleza katika mwezi wa Juni 2020, nyumba takribani 164, kati ya 210 zilikwisha uzwa kwa maana hiyo kati ya hizo zimebaki nyumba 46.

Kwa kuwa ni jambo jema, ipo haja wananchi kuipongeza ZSSF na serikali kuu, kwa hatua madhubuti iliyofikia katika kukamilisha ujenzi huo ambapo kila nyumba moja iliuzwa kwa mwananchi wa Tanzania.

Tunaipongeza serikali kwa kuweza kusimamia vyema na kuhakikisha kwamba Zanzibar nayo inakuwa kiuchumi na kufaidi matunda ya uchumi wa kati.

Inawezakana kabisa ZSSF kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar walisimamia vyema zoezi la kuuzwa kwa nyumba 164, ingawaje ingekuwa vyema kama vyumba hizi wamengeuziwa wafanyakazi ambao ndio wateja wakuu wa mfuko wa hifadhi ya Jamii Zanzibar.