NA KHAMISUU ABDALLAH

MFUKO wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), umewaomba wawekezaji mbalimbali kufuata sheria za mfuko huo kujisajili na kuwasajili wafanyakazi wao, ili kuepusha matatizo yasiyokuwa ya lazima.

Kauli hiyo imetolewa na Meneja Huduma kwa wateja kutoka mfuko huo, Khamis Filfil Than,i wakati akizungumza na wamiliki wa vyombo vya usafiri baharini na viongozi wa vyama vya wafanyakazi katika ukumbi wa Kariakoo ikiwa ni wiki ya huduma kwa wateja.

Alisema jambo hilo ni takwa la kisheria kifungu cha 5 cha sheria ya mfuko huo namba 2 ya mwaka 2005, kwa kuona kila muajiri anasajili tasisi yake kuwa mwanachama na kusajili wafanyakazi wake kujiwekea akiba pale wanapostaafu kuona wananufaika na mfuko huo.

Aidha, alisema zipo baadhi ya tasisi bado hazitaki kufuata sheria hiyo kwa kutizama michango wanayoitoa katika mfuko huo kama ni kodi.

Meneja huyo, alisema lengo la mfuko huo ni kuihifadhi jamii inayofanya kazi kuona pale inapostaafu inapata mafao yake ambayo yatawasaidia katika kuendesha maisha yao.

Alisema ZSSF inatoa mafao mbalimbali ikiwemo fao la uzeeni, mafao ya urithi, mafao ya matibabu na fao la uzazi kwa wanachama wanawake pale wanapojifungua.

Aidha, alisema ili kufanikisha hayo ni lazima kumtambua muajiri na muajiriwa, ili kupata michango yao ambayo itaweza kuwasaidia pale watapomaliza muda wa kustaafu.

Khatib Iddi Khatib kutoka kitengo cha usuluhishi na ukaguzi ZSSF, alisema zipo kampuni za usafiri ambazo zimesajiliwa na ambazo hazijasajiliwa kisheria.