NA WAANDISHI WETU

WANANCHI wa Zanzibar, wamewapongeza Marais wateule wa Jamhuri ya Muungano, wa Tanzania, John Pombe Magufuli na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, kwa kushinda uchaguzi na kuteuliwa kushika nafasi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Wananchi hao waliyasema hayo wakati wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti, kufuati ushindi walioupata katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Walisema kura walizopata washindi hao zimeashiria kukubalika kwao kwa wananchi juu ya sera walizozieleza katika kampeni.

Zaidi Ali Khamis, Mkaazi wa Kilimani, alisema kura alizopata Rais Magufuli zilizofikia 12,516,252 ikiwa ni sawa na asilimia 84.4 kati ya kura halali 14,830,195, na Dk. Hussein Mwinyi, aliyefikia kura 380,402 sawa na asilimia 76.27%.    zimeonesha wazi namna wananchi walivyowakubali ikilinganishwa na vyama vya upinzani.

Alisema kitendo cha Wapinzani wakuu katika uchaguzi huo kuambulia asilimia ndogo ya kura zote zilizopigwa zimeonesha wazi kuwa bado vyama vya upinzani havina nguvu ya kukizidi Chama cha Mapinduzi, kutokana na sera walizokuwa wakizitangaza.

“Vyama vya upinzani vimeshidwa kujiuza vizuri kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania bara katika uchaguzi huo, mgombea wa upinzani Maalim Seif wa ACT Wazalendo, amepata kura 96,103 sawa na 19.87% na Mgombea wa CHADEMA Tundu Lissu alipata kura 1,933,271 huku Bernard Membe kutoka Chama cha ACT-Wazalendo akiwa amepata kura 81,129, jambo ambalo linaonesha wazi kuna udhaifu”, alisema.

Alisema ushindi wa wagombea hao umeonesha nuru ya matumaini ya maendeleo kwa wananchi wa pande zote mbili na kinachohitajika hivi sasa ni kuona namna bora ya uongozi utavyoweza kufanya kazi kwa yale waliyoyaahidi.

Naye mwananchi mkaazi wa Kikwajuni, Saleh Akida Saumu, alisema wanakubaliana na matokeo yaliyotolewa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar, kwani yameonesha uwezo mzuri wa uongozi aliokuwa nao mgombea wa CCM.

Alisema uchaguzi mkuu umemalizika na kinachohitajika hivi sasa ni kumuunga mkono mteuliwa wa Urais huyo, ikiwa ni sehemu itayomsaidia kufanyakazi zake vizuri na kutimiza ahadi zake.

Nao wananchiwa jimbo la Makunduchi wamempongeza mgombea wa urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi, kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi katika uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28 mwezi huu.

Wakizungumza katika ofisi za Wilaya huko Makunduchi Katibu wa UWT Wilaya ya Kusini, Sihaba Fadhil Pandu, alisema mgombea huyo amekubalika kwa wananchi katika sehemu zao hasa pale alipokuwa akiomba ridhaa katika kampeni zake kwa Unguja na Pemba.

Alisema wananchi wa jimbo hilo wametekeleza kile walichomuahidi mgombea kuwa kusini itaendelea kusimamia chama cha Mapinduzi kwa lengo la kupata maendeleo.

“Siku alipokuja mgombea kuzungumza na wazee katika ofisi hizi za wilaya Makunduchi tulimuahidi kuwa Kusini itaendelea kuwa ngome ya CCM na chama kitaendelea kushika hatamu tumelitekeleza”, alisema.

Akizungumzia wawakilishi, wabunge, pamoja na madiwani alisema wananchi hawakufanya makosa katika kuhakikisha chama cha Mapinduzi kinapata wagombea watakaotekeleza Ilani ya Chama chao kupitia ngazi hizo.

 Katibu wa Umoja wa Vijana UVCCM Wilaya ya Kusini Unguja Ameir Abdalla Uchicheme, alisema wanachama wa Chama cha Mapinduzi wamefanya jitihada kubwa kwa ajili ya kukipatia ushindi wa kishindo kwa kuwachagua viongozi wa CCM.

Alisema CCM ndio chama kinachotekeleza ahadi zake, hivyo ni vyema kumuunga mkono Rais Mteule, ili kuendeleza pale alipoachiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.

“Lililobaki kumuombea dua kwa Mwenyezi Mungu katika kutekeleza ilani ya chama cha Mapinduzi kwa zile ahadi alizozitoa kwa wananchi na wanachama katika kuomba ridhaa wakati wa kipindi cha Kampeni”, alisema.

Kwa upande wa wanachama wa CCM Mkoa huo walisema wataendelea kulinda Mapinduzi ya 1964, na Muungano wa Tanzania, kwani ndio yaliyowakomboa, sambamba na kuenzi na kukitumikia chama kwa maslahi yao na Taifa.

Katika matokeo ya urais jimbo la Makunduchi jumla ya kura zilizopatikana  ni 16,502 na kwa upande wa jimbo la Paje kura zilizopatikana ni 11,906.