NA JAALA MAKAME, ZEC

TUME ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), imewatangaza wajumbe 18 kutoka Chama cha Mapinduzi kwa nafasi ya viti maalum vya Wanawake vya ujumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Tume imetangaza majina ya Wajumbe hao katika mkutano wake uliofanyika Novemba 7 mwaka huu uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Tume hiyo uliopo Maisara mjini Zanzibar.

Tume ya uchaguzi ya Zanzibar imewatangaza wajumbe 18 kutoka Chama cha Mapinduzi kwa mujibu wa masharti na maelekezo ya ibara ya 67 ya katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Aidha Tume imewatangaza wajumbe hao baada ya kuridhika kuwa wote wana sifa ya kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kama zilivyoainishwa katika katiba ya Zanzibar ibara ya 68.

Waliotangazwa na Tume ya Uchaguzi ni pamoja na Panya Ali Abdallah, Bihindi Hamad Hassan, Salma Mussa Bilali, Shadya Mohammed Suleiman, Fatma Ramadhan Mohamed (Mandoba), Sada Ramadhan Mwenda na Mwantatu Mbaraka Khamis.

Wengine ni Zainab Abdalla Salum, Riziki Pembe Juma, Leila Muhamed Mussa, Salha Mwinyi Juma, Hudhaima Mbarak Tahir, Sabiha Filfil Thani, Aza Januar Joseph, Mwanaid Kassim Mussa, Mgeni Hassan Juma, Mwanajuma Kassim Makame na Rahma Kassim Ali.

Tume tayari imeshawasilisha majina ya wajumbe hao kwa katibu wa Baraza la Wawakilishi kwa ajili ya hatua nyengine za kisheria.