NA ABOUD MAHMOUD

MICHEZO mbali mbali ya jadi, ngoma ,muziki na sanaa ni miongoni mwa mambo yanayoitambulisha jamii na kutoa mwanga juu ya utamaduni wa nchi.Zanzibar inasifika kuwa na utajiri mkubwa katika fani hizi kwa watoto, vijana na wazee.

Watu wa Zanzibar wanasifika katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa mengi katika sanaa kwa mfano mchezo wa kitendawili, mafumbo. Mashairi na utenzi umefundisha watu mambo mengi mbali ya kutoa burdani. 

 Hali hii ndio  mara nyingi hupelekea  nchi yetu kutumia njia hizi wakati tunapowakaribisha wageni mbali mbal ili waelewa mila, utamaduni na asili yetu.

Mbali na hayo utamaduni huu unawapa watu furaha, husaidia kuwaweka watu pamoja na wakati mwengine hutumika kutoa elimu au ujumbe kwa mtu, kikundi au jamii.

 Kwa mfano, unapozitafakari nyimbo zinazoimbwa wakati wa sherehe za harusi utaona wazi kwamba baadhi yao huwa zinatoa salamu na ujumbe kwa maharusi, wana wa familia na marafiki wa  maharusi.

Nchi nyingi zimefanikiwa kufika katika kujitangaza vyema kupitia njia hizi ambazo hupendwa na jamii na hasa vijana.

Hivi karibuni, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Hassan Mwinyi aligusia wakati  alipozindua Baraza la 10 la Wawakilishi  hapo Chukwani, nje kidogo ya mji wa Unguja.

Dk. Mwinyi aliahidi kuleta mabadiliko katika sekta ya michezo na utamaduni ili Zanzibar ipate mafanikio makubwa, kama alivyoahidi katika mikutano yake ya kampeni katika maeneo mbali mbali.

Kauli hiyo imewavutia wananchi wengi, hasa wanamichezo na wasanii wa fani mbali mbali, na wengi kuelezea matumaini makubwa ya kupata mafanikio yatayoweza kuwaondoshea adha tafauti walizonazo.

Dk. Mwinyi aliwahakikishia Wazanzibari kwamba atafanya kila juhudi kulinda na kukuza utamaduni wetu na michezo mbali mbali.

Hii ni pamoja na muziki wa taarab,kizazi kipya, sanaa ya filamu na matamasha mbalimbali, kama ya siku ya Utamaduni wa Mzanzibari, Sauti za busara na ZIFF ambayo yamekua mstari wa mbele kuenzi utamaduni wetu na kuinua pato na nchi.