NA MWANTANGA AME

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza a Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi, ameliapisha Baraza lake la Mawaziri, ambapo katika kuifanya kazi hiyo, amewataka Mawaziri hao kuzingatia maagizo 13, aliyoyatoa baada ya kuwaapisha.

Kati ya Maagizo hayo limo suala la usafi katika Mawizara pamoja na Mji wa Zanzibar, kwani haridhishwi na hali ilivyo hivi sasa.

Dk. Mwinyi alisema kwamba Wizara na Ofisi baadhi ni Chafu. Ofisi zisiwe kama Stoo, Maeneo ya Kazi yawe safi. Mji ni mchafu haina hadhi. Itafutwe njia mbadala ya kubadilisha hali hii.

Wakati hilo likiwa wazo la Rais, lakini ndani ya wiki hii nae  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdalla, alizitembelea Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira pamoja na Idaya ya Mazingira hapo Maruhubi.

Makamu wa Rais katika ziara yake hiyo alisisitiza na kusema kwamba pamoja na jitihada kubwa inayoendelea kuchukuliwa, lakini bado Elimu ya utunzaji wa Mazingira haijakidhi lengo.

Alisema hali ya mazingira  inaweza kuwa mbaya zaidi kama hakutachukuliwa jitihada za ziada za kudhibiti uchafuzi wa mazingira kutokana na jinsi yanavyoharibiwa na baadhi ya Watu kwa kisingizio cha kutafuta riziki ambayo inakuwa sio ya halali.

Hemed aliwataka Maafisa wa Mazingira wa Wilaya na Mikoa kuongeza jitihada zitakazosaidia nguvu kubwa ya kudhibiti  kuenea kwa uchafuzi wa Kimazingira katika maeneo yanayowazunguuka.

Aliwaomba Maafisa hao kwa kushirikiana na Wataalamu wa Mazingira kujitahidi kufanya upembuzi wa Kimazingira katika Miradi Mipya, inayoanzishwa hasa kwa  ile ya Sekta Binafsi na Uwekezaji, ili kujiepusha mapema na hitilafu za kimazingira kwenye Miradi hiyo.

Alieleza kwamba yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana kwa Miradi ya Taasisi za Serikali,  na hii imepatikana kutokana na ushauri uliotolewa na Wataaamu wa Fani hiyo ya Mazingira.

Mawazo ya viongozi hao  nafikiri yanahitaji kuungwa mkono kwani muda mrefu tumekuwa tukitumia kalamu zetu kuelezea tatizo la uchafu unaozizonga maofisi za serikali na hasa Idara.

Hii ni kutokana na ushahidi unaoonekana katika Idara za Seriikali hali ya usafi haiko vizuri, kwani baadhi ya taasisi hadi leo zina choo kimoja huku kukiwa na kundi la wafanyakazi wanaofikia 100 huku vikiwa katika mazingira machafu.

Hilo ni kutokana na maeneo hayo kutowekewa mkazo wa usafi na badala yake usafi unafanywa kwa ajili ya Mkurugenzi wa taasisi ama Katibu Mkuu ambao mara nyingi hujengewa vyoo vyao ndani ya ofisi wanazozitumia kwa shughuli zao na sio choo cha pata sote.

Vyoo hivyo, hufanyiwa usafi tofauti la vile vya pata sote kwani huwekewa aina zote za sabuni za kusafishia na vipoza harufu chafu kwa kuwekewa ‘Air Fresh’ huku ofisi zikiwa na meza, viti vilizochoka na chumbani kwa bosi kukiwa na thamani zenye gharama kubwa na sakafu zao zikiwekewa vigae vya marumaru.  

Hali hiyo, imeonekana kuwa mbaya zaidi nje ya majengo hayo ambayo yameandamwa na uchafu ikiwemo misitu na ukungu katika kuta kwa kile kilichozoeleka kama kupakwa rangi basi iwe pale kunapokuwa na sherehe maalum zikiwemo za Mapinduzi, ama Mkuu wa Nchi anapokuja kutembelea taasisi hiyo kama kufungua mradi.

Kutokana na ukweli huo, vile vile, katika barabara za mji nako hakuko vizuri, kwani unaweza kutembea mji zima hukuti hata sehemu ya kutupa taka, jambo ambalo linachangia kuifanya jamii kuona uchafuzi wa mji ni jambo la kawaida na ndio maana hawaoni tabu kutupa taka popote.

Ufanyaji wa usafi nao hauko vizuri, kwani wanaopewa kazi ya kusafisha wengi hawana vifaa vya kisasa na huku huduma hizo walikabidhiwa kwa sekta binafsi hawako vizuri kwani inawezekana ikawa ni tenda ya mtu ya kupata fedha.

Hili linawezekana kwani mara nyingi husikia taasisi husika zimeimarisha suala hilo kwa kuvipa ajira vikundi vya usafi wa sekta binafsi, lakini wanaopewa kazi hizo hawaonekani kama kweli ni taasisi, ila wanaofanya vizuri ni wale waliopewa kazi za kusafisha maofisi hasa mabenki.

Upande wa wazoaji wa taka nako kunahitaji kubadilika kwani kila leo majaa yanajaa na taka kushindwa kuondolewa kwa wakati, na sababu kubwa ni ukosefu wa magari ya kubebea taka huku yanayofanyakazi hayana mafuta ya kutosha.

Ingawa sababu hizo haziwezi kuepukika, lakini kinachoshangaza kuona magari ya watu binafsi ndio huchukua nafasi ya kubeba taka, ambayo hukodiwa kwa fedha nyingi kuifanya kazi hiyo, kwani kama yangetengenezwa basi gharama hizo zisingefikia.

Ikiwa huo ndio ukweli nafikiri tamko hili la Rais na Makamu wa Rais, lilistahili kutolewa na sasa linahitaji kufanyiwa kazi kwani ni ukweli usiopingika Mji wa Zanzibar ni mchafu na unahitaji mabadiliko makubwa yafanyike na sio kuendeleza nyimbo hii ikaendelea kuitikiwa tuu.

Hili ni jambo la msingi kwani imekuwa ni mazoea kwa baadhi ya watendaji kuona kuwajibika ni pale kiongozi hasa Rais anapotoa maagizo, wakati walitakiwa kufanya kazi hiyo kma vile walivyoomba na sio kusimamiwa.

Nafikiri Rais ameshaonesha njia ya kuwakumbusha watendaji katika taasisi kuona umuhimu wa kubuni mbinu mpya kwa kutumia wataalamu katika taasisi zao na sasa Mabaraza ya Halmashauri yanatakiwa kujiongeza kwa kuacha kutumia mbinu za kizamani kusafisha Mji na kuja katika mfumo wa kisasa zaidi.

Hili ni jambo la msingi kuliangalia hivi sasa kwani usafi wetu bado tunaufanya kwa kutumia fagio za njukuti wakati tunajua sasa hivi kuna mashine za magari ya usafi, ambazo zinaufanya mji kupendeza na sio kusubiri kuandika bajeti za kukua mabero na mapauro.

Kwa vile yapo mengi nafikiri kauli za viongozi hawa ziwe dira nzuri ya kubadilika na sio kuzifanya kama vile ‘Debe tupu, haliachi kupiga kelele’